About Me

header ads

TANZANIA BLOGGERS NETWORK , PSSSF WAJENGA USHIRIKIANO WA KUONGEZA ELIMU YA HIFADHI YA JAMII

Na mwandishi wetu , Dar es Salaam
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umefungua ukurasa mpya wa ushirikiano na Tanzania Bloggers Network (TBN), katika hatua inayolenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu hifadhi ya jamii, pensheni na uwekezaji.

Hatua hiyo imekuja baada ya ujumbe wa maofisa waandamizi kutoka PSSSF kufanya ziara katika makao makuu ya muda ya TBN, Kijitonyama jijini Dar es Salaam, ambapo walifanya mazungumzo ya kimkakati na viongozi wa mtandao huo.Mazungumzo hayo yalijikita katika kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili, hususan katika eneo la habari, elimu kwa umma na usambazaji wa taarifa sahihi kuhusu mifumo ya pensheni na uwekezaji

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, alisema mtandao huo uko tayari kutumia nguvu ya wanablogu na majukwaa ya kidijitali kuwafikishia wananchi elimu sahihi na inayoeleweka kuhusu hifadhi ya jamii.

Hata hivyo, alisema mafanikio ya mpango huo yanategemea pia wanachama wa TBN kuwa na uelewa mpana kuhusu shughuli na uendeshaji wa PSSSF.

“Tuko tayari kusimama kidete kama chombo cha kutoa elimu na kusambaza maarifa sahihi kwa umma. Lakini ni muhimu wanachama wetu wenyewe wapatiwe kwanza mafunzo ya kina kuhusu shughuli na uendeshaji wa PSSSF,” alisema Msimbe.

Alisema mafunzo hayo yatawawezesha wanablogu kutoa taarifa zenye usahihi, weledi na zinazoweza kujibu maswali ya wananchi kuhusu mafao, pensheni na masuala mengine yanayohusiana na hifadhi ya jamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa msafara wa PSSSF, Abdul Njaidi, alisema ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za kujenga uhusiano wa karibu zaidi na wadau wa sekta ya habari ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa elimu kwa jamii.

Alisema PSSSF imetambua nafasi kubwa ya majukwaa ya kidijitali katika kufikisha ujumbe kwa wananchi wengi kwa wakati mmoja.

“Lengo letu ni kujenga uhusiano wa karibu na wadau wa habari pamoja na kutoa elimu kwa jamii. Maombi na hoja zote zilizowasilishwa na TBN tutazifanyia kazi,” alisema Njaidi.

Ameongeza .

“Tunataka kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mpana na sahihi kuhusu masuala ya pensheni pamoja na uwekezaji unaofanywa na PSSSF.”

Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi, alisema mtandao huo una historia kubwa katika sekta ya habari za kidijitali nchini na unajivunia weledi wa wanachama wake.

Michuzi alisema TBN imejikita katika kuhakikisha Tanzania inapata taswira nzuri katika medani za kidijitali, huku ikichochea maendeleo kupitia taarifa na maarifa yanayowafikia wananchi kwa wakati.

“TBN ipo kwa ajili ya kuhakikisha Tanzania inasomeka vyema katika medani za kidijitali ili kuchochea na kutanua zaidi gurudumu la maendeleo ya taifa,” alisema Michuzi.

Naye Katibu wa TBN, Rahel Pallangyo, alisema mtandao huo uko tayari kushirikiana na PSSSF kwa kutumia waandishi na wanachama wake wenye uzoefu katika kuandaa na kusambaza maudhui ya elimu kwa umma.

Alisema majukwaa mbalimbali ya TBN yatatumika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, zinazoaminika na zinazoweza kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii.

“Tuko tayari kutoa waandishi wetu mahiri na kutumia majukwaa yetu mbalimbali kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na za kuaminika,” alisema Pallangyo.

Kwa ujumla, ushirikiano huo unatazamiwa kuwa chachu ya kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiandaa kwa maisha ya baada ya kustaafu, mafao yanayotolewa na mifuko ya hifadhi ya jamii, pamoja na namna uwekezaji unavyoweza kuchangia ustawi wa wanachama.

Kupitia nguvu ya vyombo vya habari vya mtandaoni na mitandao ya kijamii, PSSSF na TBN wanatarajiwa kufungua njia pana zaidi ya kufikisha elimu hiyo kwa wananchi, hususan kizazi kinachotumia zaidi majukwaa ya kidijitali kupata habari na maarifa.

Katika mkutano huo, ujumbe wa PSSSF ulioongozwa na Abdul Njaidi ulijumuisha maofisa Regina Kumba, Grayson Mgunda na Doreen Lyimo.

Kwa upande wa TBN, viongozi walioshiriki ni Mwenyekiti Beda Msimbe, Katibu Rahel Pallangyo, Mtaalamu wa Mawasiliano Cathbert Kajuna pamoja na Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi.

Ushirikiano huu mpya unaweka msingi wa kutumia nguvu ya habari za kidijitali kama daraja kati ya PSSSF na wananchi, kwa lengo la kuhakikisha elimu ya hifadhi ya jamii haibaki kwenye taasisi pekee, bali inawafikia wananchi kwa lugha rahisi, sahihi na inayoeleweka.





Post a Comment

0 Comments