
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray, amemtaka Mkandarasi wa mradi wa Mikocheni Apartments kuongeza kasi ya ujenzi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika ifikapo Oktoba mwaka huu.
Mhe. Qwaray ametoa maelekezo hayo leo, Agosti 7, 2026 alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo jijini Dar es Salaam, ambao unasimamiwa na kumilikiwa na Watumishi Housing Investments.
Amesema Serikali inatarajia kuona Mkandarasi akiweka nguvu zaidi katika kukamilisha mradi huo kwa wakati ili watumishi wa umma ambao tayari wamelipia nyumba hizo waanze kuzitumia.
“Pamoja na kukamilisha mradi kwa wakati, Mkandarasi anapaswa kuzingatia viwango vya ubora wa ujenzi ili nyumba zinazojengwa zidumu na Serikali iweze na kuona thamani ya fedha iliyowekezwa” amesema.
Sambamba na hayo, Mhe. Qwaray ametoa wito kwa watumishi wa umma na wananchi wenye sifa ya kujiunga na Mfuko wa Faida Fund ili kujenga akiba ya muda mrefu itakayowawezesha kuwa na uhakika wa kifedha hapo baadaye.
Aidha, amesema kwa watumishi wa umma kujiunga na mfuko huo kutawasaidia kuongeza mafao yao ya uzeeni bila kuathiri mafao ya msingi yanayolipwa kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii, huku akisisitiza kuwa uwekezaji wa mapema ni msingi wa ustawi wa kifedha.
“Sisi maelekezo ya Waziri tumeyapokea na tutaendelea kumsimamia mkandarasi ili aweze kukamilisha nyumba hizi kwa wakati, kama mkataba unavyotaka,” alisema.




0 Comments