About Me

header ads

HUDUMA ZA PPAA ZAMKOSHA WAZIRI ULEGA

Na Mwandishi Wetu, Dar

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb.) amefurahishwa na Huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) hususan matumizi ya Moduli ya kupokea na kushughulukia malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST. 

Waziri Ulega ameipongeza PPAA alipotembelea banda la Mamlaka hiyo pembezoni mwa Mkutano wa Mashauriano na Wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa Mwaka 2026 unaofanyika tarehe 13 – 14, Agosti, 2026 Jijini Dar es Salaam. 

PPAA imeshiriki maaonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu juu ya huduma mbalimbali inazozitoa kwa wadau wa ununuzi wa umma hususan matumizi ya Moduli ya kupokea na kushughulukia malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST. 

Hongereni kwa kazi nzuri ya kutoa elimu kwa wadau wenu hasa wakandarasi walioshiriki katika mkutano wa leo, endeleeni kufanya kazi hii nzuri ili kutimiza azma ya Serikali ya kuwasogezea wananchi huduma kwa karibu zaidi,” amesema Mhe. Ulega 
Kwa Upande wake Mkuu wa Sehemu ya Huduma za Sheria PPAA, Bi. Agnes Sayi ambaye alimwakilisha Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando alimweleza Waziri Ulega kuwa kuanza kwa matumizi ya Moduli ya kupokea malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST kumechangia kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi kwenye mnyororo wa ununuzi na ugavi. 

“Mhe. Waziri matumizi ya moduli katika mnyororo wa ununuzi na ugavi yamechangia kutoa maamuzi kwa haki na wakati na kuwezesha miradi ya Serikali kutekelezwa kwa wakati,” amesema Bi. Sayi

Pamoja na mambo mengine, Bi. Sayi amemweleza Mhe. Ulega kuwa  kwa sasa PPAA inatoa huduma ya Mkutano kwa njia ya Mtandao “Video Conference” ambapo hutumika kusikiliza mashauri ya wazabuni walioshindwa kufika katika Ofisi za Mamlaka ya Rufani kwa ajili ya kusikiliza rufaa zilizowasilishwa.

“Huduma ya ‘video conference’ inatoa fursa ya kuwasikiliza wazabuni walioshindwa kufika PPAA na hivyo kuiwezesha Mamlaka ya Rufani kutekeleza jukumu lake la msingi la utatuzi wa migogoro itokanayo na michakato ya ununuzi wa Umma kwa haki na wakati,” ameongeza Bi. Sayi

Awali akifungua Mkutano wa Mashauriano na Wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa Mwaka 2026 unaoendelea Jijini Dar es Salaam, Waziri Ulega amewataka Wakandarasi wazawa na wakandarasi wote nchini kwa ujumla kuhakikisha kuwa wanatekeleza miradi wanayoipata kwa weledi na ufanisi.

Aidha, Waziri Ulega ameongeza Serikali imeandaa mikakati ya kuwasaidia Wakandarasi wazawa na Washauri Elekezi ili waweze kunufaika kupitia miradi inayotolewa nchini na kuwataka watendaji wa Wizara ya Ujenzi kutoa ushirikiano na kuhakikisha wanatatua changamoto zinazowakwamisha wakandarasi wa ndani kupata miradi.

Mkutano wa Mashauriano na Wadau wa Sekta ya Ujenzi, umeongozwa na Kaulimbiu, “Dira 2025: Fursaa na Wajibu wa Makandarasi katika ujenzi wa Miundombinu Endelevu”


 

Post a Comment

0 Comments