Akizungumza kuhusu fursa hizo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa BMT, Bw. Aminiel Aligaesha, amesema AFCON 2027 ni tukio la kihistoria litakalofanyika kwa mara ya kwanza Ukanda wa Afrika Mashariki na likiwa linatimiza miaka 70 mwakani tangu kuanzishwa kwake.
Kwa mujibu wa Bw. Aligaesha, fursa ya kwanza ni kuongezeka kwa biashara na shughuli za kiuchumi, ambapo hoteli, nyumba za kulala wageni, migahawa, maduka pamoja na wauzaji wa bidhaa zenye nembo za mashindano watanufaika kutokana na ongezeko la wageni na mashabiki.
Aidha, amesema sekta ya benki na huduma za kifedha itanufaika kupitia ongezeko la miamala ya kifedha, huduma za kubadilisha fedha za kigeni, udhamini wa matukio na utoaji wa bidhaa maalum za kifedha kwa wafanyabiashara watakaohudumia wageni.
Katika upande wa ajira, Bw. Aligaesha amesema vijana watapata nafasi za kazi katika sekta za ukarimu, usafiri, utalii, teknolojia, uandishi wa habari, uzalishaji wa maudhui na huduma nyingine, hali itakayowaongezea uzoefu wa kufanya kazi katika mazingira ya kimataifa.
Pia ametaja sekta ya usafiri kuwa miongoni mwa zitakazonufaika kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya usafiri wa anga, nchi kavu na majini, ikiwemo safari za ndani, huduma za teksi, mabasi, usafiri wa mtandaoni na vifurushi maalum vya safari za AFCON vinavyoweza kujumuisha utalii na malazi.
Kwa mujibu wa Bw. Aligaesha, AFCON 2027 pia itachochea maendeleo ya soka nchini kwa kuhamasisha uwekezaji katika akademi za vijana, ukocha, urefa na ukuzaji wa vipaji, huku sekta ya afya ikitarajiwa kunufaika kupitia utoaji wa huduma kwa wageni na kukuza utalii wa afya kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali.
Amesema mashindano hayo yatatoa jukwaa la kutangaza utamaduni wa Tanzania kupitia muziki, vyakula, sanaa, mavazi na lugha ya Kiswahili, sambamba na kuitangaza Tanzania (national branding) kwa mamilioni ya watazamaji duniani kupitia televisheni, mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya kimataifa.
Kuhusu sekta ya utalii, Bw. Aligaesha alisema wageni watakaokuja kushuhudia mashindano hayo watapata nafasi ya kutembelea vivutio mbalimbali ikiwemo Serengeti, Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na Zanzibar, jambo litakaloongeza mapato ya sekta hiyo.
Ameongeza kuwa maandalizi ya AFCON tayari yamechochea maboresho makubwa ya miundombinu ikiwamo ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, ujenzi wa viwanja vipya Arusha na kule Zanzibar, pamoja na uboreshaji wa barabara, viwanja vya mazoezi na mifumo ya huduma za kidijitali ambayo itaendelea kutumika hata baada ya mashindano hayo kumalizika.
Kwa mujibu wa Bw. Aligaesha, mafanikio ya maandalizi na uendeshaji wa AFCON 2027 yataifanya Tanzania kuwa kitovu cha michezo barani Afrika, huku yakifungua milango ya kuandaa mashindano mengine ya kimataifa, kuvutia wawekezaji na kukuza uchumi wa michezo.
Aidha, amesema mashindano hayo yataimarisha diplomasia ya michezo na ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na kuimarisha uhusiano wa kikanda katika biashara, utalii, utamaduni na uwekezaji.
Akihitimisha, Bw. Aligaesha amewataka Watanzania kuendelea kufuatilia taarifa za BMT, akieleza kuwa utaratibu rasmi wa namna wananchi na wadau watakavyoweza kushiriki na kunufaika kupitia fursa hizo utatangazwa baadaye mwaka huu.
"Tunatoa wito kwa wananchi, wafanyabiashara na wadau wote kuanza kujiandaa mapema. AFCON 2027 ni mwanzo wa ukurasa mpya wa maendeleo ya michezo na uchumi wa michezo nchini, na muda si mrefu tutatangaza utaratibu wa namna fursa hizi zitakavyopatikana," amesisitiza Bw. Aligaesha.


0 Comments