About Me

header ads

WAZIRI MKUU AFANIKISHA MARIDHIANO YA MGOGORO WA MIAKA 14 KATI YA MARTHA HILONGA NA KANISA KATOLIKI ARUSHA

Utaratibu wa Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa njia ya mazungumzo na maridhiano umewezesha kupatikana kwa suluhu ya mgogoro wa miaka 14 kati ya Bi. Martha Hilonga wa Mto wa Mbu mkoani Arusha na Parokia ya Mtakatifu Yuda Thadei ya Kanisa Katoliki Mto wa Mbu, Jimbo Kuu Katoliki la Arusha.

Mgogoro huo ulianza mwaka 2012 baada ya Bi. Martha Hilonga kupata ajali iliyohusisha gari la Parokia hiyo, hali iliyosababisha kupoteza mguu wake wa kulia. Tangu wakati huo, jitihada za kutafuta fidia kupitia vyombo mbalimbali ikiwemo Mahakama ziliendelea kwa miaka mingi bila kufikia suluhu ya kudumu.

Mwezi Februari 2026, wakati wa mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi uliofanyika Mto wa Mbu wilayani Monduli, Bi. Martha aliwasilisha malalamiko yake kwa Waziri Mkuu akieleza kuwa licha ya kufuatilia haki yake kwa muda mrefu, bado hakuwa amepata fidia .

Baada ya kupokea malalamiko hayo, Waziri Mkuu alielekeza timu ya wataalamu kutoka Ofisi yake kwenda mkoani Arusha kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro huo kwa njia ya maridhiano. Timu hiyo ilifanya mazungumzo na Bi. Martha, viongozi wa Serikali, viongozi wa Kanisa Katoliki pamoja na wanasheria wa pande zote katika vikao vilivyofanyika kwa kipindi cha wiki mbili.

Mazungumzo hayo yalihitimishwa kwa makubaliano ya pande zote kuondoa shauri lililokuwa Mahakama ya Rufani na kumaliza mgogoro huo kwa njia ya maridhiano.

Katika maridhiano hayo, Jimbo Kuu Katoliki la Arusha lilikubali kumjengea Bi. Martha nyumba ya kuishi kutokana na athari za ulemavu wa kudumu alioupata kufuatia ajali hiyo.

Aidha, Waziri Mkuu ameahidi kumwezesha Bi. Martha kupata mtaji wa biashara utakaomsaidia kujitegemea kiuchumi. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa na pande zote, Kanisa Katoliki litajenga nyumba yenye vyumba viwili vya kulala, sebule, jiko na choo cha ndani katika kipindi kisichozidi miezi sita.

Akizungumza baada ya kufikiwa kwa maridhiano hayo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Isaac Aman amesema Kanisa linaamini katika utu, upendo na mshikamano wa kijamii na kwamba litatekeleza makubaliano hayo kwa wakati ili kumaliza kabisa mgogoro huo.

Naye Bi. Martha Hilonga ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kusikiliza kilio chake na kufanikisha kupatikana kwa suluhu ya mgogoro uliodumu kwa miaka 14.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Bw. John Lawena amesema Kanisa litazingatia na kutekeleza kwa wakati masharti yote yaliyobainishwa katika nyaraka za maridhiano.

Maridhiano hayo yamehitimisha mgogoro uliodumu kwa zaidi ya muongo mmoja na kuwa mfano wa namna mazungumzo na ushirikiano kati ya wadau mbalimbali vinavyoweza kusaidia kutatua migogoro ya muda mrefu kwa amani na kuelewana.



 

Post a Comment

0 Comments