About Me

header ads

DK.MSEMWA ATAJA MAMBO MUHIMU KUFANIKISHA UTEKELEZAJI DIRA 2050


 Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji anayeshugulikia Uwekezaji, Dkt. Fred Msemwa amesema kufanikiwa kwa utekelezaji wa Dira 2050  kutategemea sana Uwezo,ufanisi na ubunifu wa sekta ya umma.

Amesema sekta ya umma ina jukumu la kuzidi kuboresha utendaji wake kutoka shughuli za utawala wa kawaida kwenda katika utendaji wenye matokeo, utendaji unaowalenga wananchi na unaojali matokeo.

Dk.Msemwa hayo alipokuwa akizungumza njia ya mtandao wakati wa Kongamano la Pili la Utumishi wa Umma Tanzania 2026 lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNCC) jijini Dar es Salaam,

Akieleza zaidi wakati wa kongamano hilo amefafanua  pia kuna mambo matano zaidi ya kuweza kuyafanyiwa kazi zaidi ili kuimarisha utekelezaji wa Dira 2050.

Ametaja jambo la  kwanza ni kuchochea  utamaduni wa uvumbuzi ambapo amesema sekta ya umma lazima iweke mazingira ya kuweza mawazo mapya na majawabu mapya kwa matatizo ya wananchi. Ni muhimu kuongeza ushirikiano na vyuo, taasisi za utafiti pamoja na sekta binafsi ili kuchochea upatikanaji wa mawazo mapya.

Pia jambo la pili ni kutoa huduma kwa kuwafikiria wananchi ambapo amefafanua mifumo ya utoaji huduma ni muhimu ilenge mahitaji ya wananchi na shughuli zao za kiuchumi. Hivyo sekta ya umma irahisishe taratibu na mifumo yake ili ifikike kiharisi. 

“Lazima kuwa na huduma  jumuishi na zinazofikika na kuwa na uwezo wa kupata mrejesho kutoka kwa wananchi.”

Wakati  jambo la tatu ni kuimarisha  ushirikiano na sekta binafsi ambapo amesema Ili kufikia malengo ya Dira2050 ambayo inaipa nafasi kubwa sekta binafsi katika kufanikisha malengo yetu ya kiuchumi. 

“Sekta ya umma ni lazima iweke mazingira bora kwa ajili ya kukuza Ujasiriamali, uwekezaji na ujenzi wa miundombinu. Ushirikiano huu ni muhimu katika kuleta si tu umoja wa kitaifa lakini pia kuzalisha ajira, kuleta ufanisi katika uzalishaji na utoaji huduma.”

Jambo la nne ni kuimarisha utaratibu wa kisera na serikali ifikirie kama mtu mmoja.Serikali imepiga hatua kubwa katika kuweka mifumo bora ya utendaji na ufuatiliaji wa shughuli zake. Ni muhimu kwa serikali kuendelea kuimarisha mifumo hiyo ili kuleta ufanisi zaidi.

Wakati jambo la tano ni kubadili mtizamo ,ambapo amesema Dira 2050 ina malengo makubwa na ufikiaji wa malengo utahitaji kufanyika kwa mambo katika utaratibu usio wa kawaida. 

“Ni muhimu kwa serikali kuendelea kufanya maboresho na kupunguza urasimu na kulenga katika kasi na ubora wa huduma. Kuhama kutoka katika mifumo inayodhibiti shughuli za sekta binafsi kwenda katika kuwezesha sekta binafsi, kuwa na mtizamo wa muda mrefu badala ya kufikiria malengo ya muda mfupi,”amesema Dk.Msemwa.

Post a Comment

0 Comments