Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Lameck Nchemba amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa, Said Majaliwa kwa usimamizi, utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Shule ya Ufundi ya Amali Kingale wilayani Kondoa mkoani Dodoma.
Pia, ujenzi wa maendeleo ya miundombinu ya shule hiyo unaotekelezwa kwa kutumia mfumo wa Force Account utasaidia kuongeza ubora wa elimu na umeshirikisha jamii kikamilifu.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Dk. Mwigulu alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika elimu ya ufundi nchini, ambapo katika kipindi cha miaka minne hadi mitano shule 103 za ufundi zimejengwa, zikiwemo shule 29 za uhandisi.
“Hii ni hatua kubwa, na hii ni awamu ya kwanza, yatajengwa majengo mengine yote ili kukamilisha seti kamili ya shule hizi. Tangu uhuru tulikuwa na shule tano tu za ufundi, lakini Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan katika miaka yake minne kwenda mitano amejenga shule 103, jambo ambalo ni kubwa sana,” alisema
Alisema "Mkurugenzi hapa umefanya vizuri na tunakupongeza kwa kazi kubwa uliyoifanya"
Akitoa maelezo kuhusu mradi huo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Dk. Festo Dugange alisema shule hiyo imepokea jumla ya Shilingi Milioni 544.2 kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi uliojumuisha ujenzi wa vyumba vya madarasa, maabara, jengo la utawala, maktaba, jengo la TEHAMA pamoja na nyumba ya mwalimu.
Dk. Dugange alieeleza kuwa Halmashauri ya Mji Kondoa ni miongoni mwa Halmashauri chache zilizobahatika kupata shule bora ya mafunzo ya ufundi, hatua ambayo amesema itasaidia kuongeza fursa za elimu ya amali kwa vijana wa eneo hilo na maeneo ya jirani.
Aidha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kondoa, Said Majaliwa aliishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huo huku akieleza kuwa ushirikiano wa wananchi umechangia kufanikisha maendeleo ya ujenzi huo, ikiwemo kutoa eneo la mradi lenye ukubwa wa ekari 20 na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya shule hiyo. Kwa mujibu wa taarifa ya mradi, shule hiyo yenye usajili namba S.6979 tayari imeanza kutoa huduma ikiwa na walimu sita (6) na wanafunzi 126.





0 Comments