About Me

header ads

MWANAFUNZI AJIFUNGULIA CHOONI NA MTOTO WA MIAKA 6 ALAWITIWA CHALINZE-MORCASE

Na Mwamvua Mwinyi-Pwan Mei 20, 2026

Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Kibindu ,Chalinze wilayani Bagamoyo, ,mkoani Pwani amejifungua mtoto wa kike kisha kumtupa kwenye shimo la choo cha mabweni ya wanafunzi wa kike, katika tukio lililoibua taharuki shuleni hapo baada ya mwanafunzi mwenzake kusikia sauti ya mtoto chooni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase alisema tukio hilo liligundulika Mei 19, 2026 majira ya saa 4:00 asubuhi katika shule hiyo . 

Alisema mwanafunzi huyo alikuwa na ujauzito ambao haukubainika katika kipindi chote cha miezi tisa kutokana na kuvaa majuba hadi alipopatwa na maumivu makali ya tumbo na kwenda chooni, ambako alijifungua mtoto huyo kabla ya kumtupa kwenye shimo la choo.

Morcase alieleza mwanafunzi mwingine aliingia chooni na kuona matone ya damu karibu na tundu la choo, na alipomwaga maji alisikia sauti ya mtoto ndipo alipotoa taarifa kwa uongozi wa shule.

Alieleza kuwa kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji pamoja na Polisi Kata, jitihada za kumuokoa mtoto zilifanyika na kukimbizwa katika Kituo cha Afya Kibindu kwa matibabu.

“Mama na mtoto wanaendelea na matibabu katika Kituo cha Afya Kibindu na baada ya matibabu kukamilika hatua nyingine za kisheria zitafuata,” alifafanua Morcase. 

Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi Mkoani humo linamshikilia Kesi Juma Ibrahim, miaka 22, mkulima na mkazi wa Kifuleta, Chalinze kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wa miaka sita (jina linahifadhiwa).

Kwa mujibu wa Kamanda Morcase tukio hilo lilitokea Mei 17, 2026 majira ya saa 7:00 mchana baada ya mtuhumiwa huyo kumlaghai mtoto ambaye ni jirani yake na kumuingiza chumbani kwake kabla ya kumfanyia kitendo hicho.

Alieleza wazazi wa mtoto walipogundua tukio hilo walitoa taarifa Kituo cha Polisi Mbwewe ambapo mtuhumiwa alikamatwa na upelelezi unaendelea kabla ya kufikishwa mahakamani.

Morcase alikemea vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa wakati ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Post a Comment

0 Comments