About Me

header ads

DKT AKWILAPO KUWAUNGA MKONO VIJANA WANAOTENGENEZA SAMANI MASASI

Na Munir Shemweta, MASASI


Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo ameahidi kukiunga mkono kikundi cha vijana cha UBINAKI kinachojishughulisha na mradi wa utengemezaji samani za majumbani na ofisini.

Mradi wa vijana wa UBINAKI unatokana na mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na Halmashauri kwa makundi ya vijana, wanawake pamoja na watu wenye walemavu ambapo vijana hao wa Masasi wameonesha ubunifu mkubwa pamoja na matumizi sahihi ya fedha walizopatiwa kwa kuanzisha shughuli yenye tija kwao na kwa jamii inayowazunguka.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi wa vijana wa UBINAKI wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa jana katika halmashauri ya Mji Masasi Dkt Akwilapo amewapongeza vijana hao kwa kuungana, kufanya kazi pamoja sambamba na kujitegemea katika kuendesha shughuli za kujitafutia kipato.

‘’Hawa ni mfano wa kuigwa na ningependa vijana wengine wote waige mfano wa vijana hawa na mimi hawa nitawaunga mkono’’ amesema Mhe. Dkt Akwilapo

Katika kuonesha dhamira ya kuwawezesha vijana hao, Mhe. Dkt Akwilapo aliahidi kununua kitanda kimoja kati ya vile vilivyotengenezwa na vijana hao ikiwa ni ishara ya kuwaunga mkono.

Aidha, aliwaambia vijana hao wa UBINAKI kuwa, katika ile pesa wanaorejesha mkopo wa asilimia 10 wa halmashauri ya Mji Masasi atawachangia kiasi cha shilingi laki nne katika kipindi cha miezi sita ya marejesho.

Amesema, uamuzi wa kuwasaidia vijana hao ni kuongeza hamasa kwa vijana wengine kuanzisha vikundi kama hivyo na yeye atawaunga mkono kwa sababu uanzishwaji vikundi vya aina hiyo utawafanya vijana kujitegemea, kuwa na kazi na kuacha kutumia muda mwingi katika michezo ya pool table na mambo mengine yasiyo na faida.

Kwa mujibu wa taarifa ya kikundi cha UBINAKI, mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya kikundi hicho ni pamoja na vijana kujiajiri kupitia shughuli za utengenezaji na uuzaji wa samani, kupata soko la bidhaa za ndani ya mkoa wa Mtwara na nje ya Mkoa pamoja na kutoa ajira kwa vijana 8.

Kikundi cha Vijana cha UBINAKI kilianzishwa tarehe 21.03.2023 kikiwa na mtaji wa shilingi 3,380,000 ikijumuisha na mashine za mkono ambazo zilitokana na michango toka kwa wanakikundi. Kikundi kilipata usajili kwa namba MTW/MAS/VIJ/2023/0044 kikiwa na wanachama 5(1Ke na 4 Me).

Halmashauri ya Mji Masasi ilikipatia mkopo wa Shilingi 30,972,000/= kikundi cha UBINAKI kupitia fedha za asilimia 10% ya mapato ya ndani. Mkopo huo umekisaidia kikundi cha vijana hao kuboresha mazingira ya kiwanda, ununuzi wa Malighafi, vitendea kazi ikiwemo Kununua mashine za kisasa mbili (2).

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi wa Kikundi cha Vijana cha UBINAKI uliofanywa wakati wa Mbio za Mwenge kitaifa katika halmashauri ya Mji Masasi mkoani Mtwara jana.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akiangalia sehemu ya Samani zilizotengenezwa na kikundi cha vijana cha UBINAKI wakati wa ukaguzi wa mradi wa Kikundi hicho uliofanywa wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika halmashauri ya Mji Masasi mkoani Mtwara jana.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2026 Bw. Michael Mwang’onda akipata maelezo ya mradi wa utengenezaji Samani unaofanywa na Kikundi cha Vijana cha UBINAKI wakati wa ukaguzi wa mradi wa Kikundi katika halmashauri ya Mji Masasi mkoani Mtwara jana. Wa tatu kulia ni Mbunge wa jimbo la Masasi Mjini na Waziri wa Ardhi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2026 Bw. Michael Mwang’onda akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi wa utengenezaji Samani unaofanywa na Kikundi cha Vijana cha UBINAKI katika halmashauri ya Mji Masasi mkoani Mtwara jana.

Post a Comment

0 Comments