Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Leonard Akwilapoamesema jumla ya wananchi 13,550 wamejitokeza kupata huduma mbalimbali za sekta ya ardhi kupitia Samia Ardhi Kliniki iliyofanyika katika mikoa yote 26 nchini.Dkt. Akwilapo amesema hayo wakati akifunga rasmi Samia Ardhi Kliniki katika viwanja vya Mashujaa mkoani Mtwara tarehe 7 Machi 2026, akisema kliniki hiyo imekuwa jukwaa muhimu la kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi hususan wanawake.
Amesema, kati ya wananchi waliojitokeza katika kliniki hizo, wanawake walikuwa 8,725 sawa na asilimia 64.4 huku wanaume wakiwa 3,892 sawa na asilimia 35.7, jambo linaloonesha mwitikio mkubwa wa wanawake katika kutumia fursa zinazotolewa na Serikali.
Aidha, Waziri Akwilapo amesema, jumla ya hatimiliki 3,131 zimetolewa kwa wananchi waliokamilisha taratibu za umilikishwaji wa ardhi ambapo hatimiliki 2,081 sawa na asilimia 57.4 zimetolewa kwa wanawake na hatimiliki 1,543 sawa na asilimia 43.6 zimetolewa kwa wanaume.
Amefafanua kuwa, hatua hiyo imeongeza usalama wa milki kwa wananchi pamoja na kuimarisha uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla.
“Ardhi ni msingi wa uchumi wa mwananchi na Taifa. Mwanamke anapomiliki ardhi kisheria anapata uwezo mkubwa wa kuwekeza, kufanya shughuli za uzalishaji na hata kupata mikopo katika taasisi za fedha,” alisema.
Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Donald Msengi amesema, Samia Ardhi Kliniki imenufaisha wanawake kwa kuwaelimisha jambo alilolieza kuwa limelenga kuwawezesha na kulinda haki na kutatua changamoto zao.
‘’Kupitia Kliniki hiyo wanawake walipewa huduma mbalimbali ambazo ni elimu ya kumiliki ardhi, ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala ya ardhi pamoja na utoaji hati’’ amesema Kanali Msengi.
Katika hatua nyingine, Dkt Akwilapo amesema, kupitia Samia Ardhi Kliniki jumla ya kero, malalamiko na migogoro ya ardhi 707 zimesikilizwa na kupatiwa ufumbuzi, huku Serikali ikikusanya kiasi cha shilingi milioni 972.16 kupitia huduma mbalimbali zilizotolewa katika kliniki hizo.
Amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira bora yanayolinda haki za wanawake kupitia maboresho ya sera na sheria mbalimbali zinazolenga kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Amesema, kupitia maboresho ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 (toleo la mwaka 2023) pamoja na Sheria ya Ardhi na Sheria ya Ardhi ya Vijiji, wanawake wameendelea kutambuliwa kisheria kumiliki, kutumia na kufanya miamala ya ardhi kwa usawa na wanaume.
Waziri Akwilapo pia amewashukuru wadau mbalimbali walioshiriki kufanikisha kliniki hiyo wakiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA) na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa wananchi.
Ameongeza kuwa, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itaendelea kuendesha kliniki za ardhi katika maeneo mbalimbali nchini ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Samia Ardhi Kliniki ilianza Machi 2, 2026 na kuhitimishwa tarehe 7 Machi 2026 ikiwa ni kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanzisha kliniki hiyo kwa lengo kuwafikia wanawake na kuwapatia elimu ya masuala ya ardhi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa kufunga Kliniki Maalum ya Samia Ardhi Kliniki katika viwanja vya Mashujaa mkoani Mtwara tarehe 7 Machi 2026.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akimkabidhi Hati Miliki ya Ardhi kwa mmoja wa wakazi wa Mtwara aliyehudumiwa wakati Samia Ardhi Kliniki katika viwanja vya Mashujaa mkoani Mtwara tarehe 7 Machi 2026.
Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Donald Msengi akikabidhi hati kwa mwananchi aliyehudumiwa wakati wa Samia Ardhi Kliniki mkoani Mtwara tarehe 7 Machi 2026.


Mkuu wa wilaya ya Mtwara Abdallah Mwaipaya akikabidhi hati milki ya ardhi wakati wa Samia Ardhi Kliniki mkoani Mtwara.

Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mtwara wakiwa katika zoezi la kuhudumia wananchi wakati wa Samia Ardhi Kliniki katika viwanja vya Mashujaa mkoani Mtwara.
Baadhi ya wananchi walioshiriki hafla ya kufunga Samia Ardhi Kliniki katika viwanja vya Mashujaa mkoani Mtwara.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (katikati) pamoja na Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Donald Msengi (wa pili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukabidhi hati milki za ardhi kwa wananchi waliohudumiwa wakati wa Samia Ardhi Kliniki katika viwanja vya Mashujaa mkoani Mtwara tarehe 7 Machi 2026. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)





0 Comments