Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Kampasi ya Tanga leo tarehe 7 Machi 2026 kimetekeleza shughuli ya kutoa huduma kwa jamii kwa kutembelea Kituo cha Afya Ngamiani kilichopo jijini Tanga. Katika ziara hiyo, chuo kimetoa msaada wa vifaa tiba pamoja na mahitaji mbalimbali ya msingi kwa watoto waliopo katika wodi ya wazazi.
Sambamba na hilo, watumishi na wanafunzi wa kampasi hiyo wakiongozwa na Mkurugenzi wa Kampasi, Bi. Zawadi Rashidi, walifanya usafi katika maeneo mbalimbali ya kituo hicho ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 25 ya chuo hicho.
Akizungumza wakati wa kukabidhi misaada hiyo, Bi. Zawadi Rashidi alisema kuwa chuo kina historia na wajibu wa kurudisha kwa jamii inayokizunguka. Alisisitiza kuwa kusaidia jamii ni sehemu ya dhima ya chuo kwa mujibu wa sera zake.
“Msaada huu unaonyesha mapenzi ya dhati kwa jamii inayotuzunguka. Pamoja na wajibu wa kutoa elimu, pia tuna jukumu la kuhudumia jamii inayotuzunguka, hasa katika kipindi hiki ambacho chuo kinasherehekea miaka ishirini na tano tangu kuanzishwa kwake,” alisema.
Aliongeza kuwa msaada uliotolewa unatarajiwa kusaidia kuboresha huduma zinazotolewa katika wodi ya wazazi pamoja na vitengo vingine ndani ya kituo hicho, ambacho kinaendelea kuhudumia wananchi wengi wa jiji la Tanga na maeneo jirani.
Kwa upande wake, Mfamasia wa Kituo cha Afya Ngamiani, Michael Mrosho, aliyepokea misaada hiyo kwa niaba ya Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, alishukuru kwa niaba ya uongozi na watumishi wote wa kituo hicho. Alisema msaada huo unaonyesha mapenzi ya dhati ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kwa jamii inayokizunguka.
“Tunawashukuru kwa msaada huu unaoonyesha upendo wenu kwa jamii, hususan wananchi wa Ngamiani. Kupitia vifaa hivi, utoaji wa huduma kwa wagonjwa utaimarika zaidi,” alisema Mrosho.





0 Comments