About Me

header ads

‘’MSITOE MAAMUZI YA KUWAFURAHISHA WATU’’- DKT AKWILAPO

Na Munir Shemweta, WANMM MTWARA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Leonard Akwilapoameshuhudia uapisho wa wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya na kuwataka wajumbe hao kutenda haki kuacha kutoa maamuzi ya kuwafurahisha watu wakati wa kusikiliza mashauri ya ardhi.

Uapisho huo umeongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Donald Wilson Msengi, na kufanyika leo tarehe 7 Machi 2026 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Akizungumza mara baada ya kushuhudia uapisho huo, Dkt. Akwilapo aliwaasa wajumbe wa mabaraza hayo kuepuka kutoa maamuzi kwa lengo la kuwafurahisha watu au makundi fulani, badala yake wafanye maamuzi yanayozingatia haki na sheria ili kupunguza migogoro ya ardhi katika jamii.

Alisema wajumbe wanapaswa kutambua kuwa nafasi waliyopewa ni dhamana kubwa kutoka kwa Mungu na Serikali, hivyo wanatakiwa kuitumia kwa uadilifu, uaminifu na kwa kuzingatia misingi ya haki.

“Napenda mtambue kuwa nafasi mlizopewa ni kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, hivyo mheshimu Mungu kwa kufanya maamuzi yanayoendana na haki na uadilifu,” alisema Dkt. Akwilapo.

Aliongeza kuwa, kazi ya kushughulikia mashauri ya ardhi si rahisi, kwani mara nyingi huwa na pande mbili zinazopingana, lakini wajumbe wanapaswa kufanya maamuzi kwa kuzingatia ushahidi na sheria ili haki ipatikane kwa anayestahili.

“Sina wasiwasi na ninyi, ingawa kazi ni ngumu, lakini mfanye maamuzi kwa kuzingatia haki na siyo kumfurahisha mtu,” alisisitiza.

Dkt. Akwilapo pia alisema uimarishaji wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa kusogeza huduma hizo karibu zaidi na wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Msengi aliwapongeza wajumbe hao kwa kuaminiwa kushika nafasi hizo na kuwataka kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia viapo walivyokula na kufanya kazi kwa weledi.

Amesema, wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya ni kiungo muhimu katika mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa uadilifu ili kujenga imani kwa wananchi.

“Uwepo wa wajumbe wa mabaraza ya ardhi katika wilaya zenu sasa utawezesha wananchi kupata huduma karibu zaidi badala ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo,” alisema.

Ameongeza kuwa, hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama na muda ambao wananchi walikuwa wakitumia kufuata huduma za utatuzi wa migogoro ya ardhi katika maeneo ya mbali.

Wajumbe walioapishwa wanatoka katika wilaya za Mtwara, Tandahimba, Newala pamoja na wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.

Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kuimarisha Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya ili kuongeza ufanisi katika kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi kwa wakati, jambo litakalosaidia kuimarisha usalama wa milki na kuleta utulivu katika jamii.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa kuapishwa kwa wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya mkoani Mtwara tarehe 7 Machi 2026.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Donald Msengi akimuapisha mmoja wa wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya mkoani Mtwara tarehe 7 Machi 2026.
Baadhi ya maofisa wa idara mbalimbali mkoani Mtwara wakiwa katika hafla ya kuapishwa kwa wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya mkoani Mtwara tarehe 7 Machi 2026.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (wa pili kushoto mstari wa mbele) na Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Donald Msengi(wa tatu kulia mstari wa mbele) pamoja na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya mkoani Mtwara walioapishwa tarehe 7 Machi 2026. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Sehemu ya Wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya mkoani Mtwara walioapishwa tarehe 7 Machi 2026
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Donald Msengi akizungumza wakati wa hafla ya kuwaapisha Wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya mkoani Mtwara tarehe 7 Machi 2026

Post a Comment

0 Comments