About Me

header ads

ACI FMA Tanzania yathibitisha kuunga mkono maendeleo ya masoko ya fedha nchini

ACI FMA Tanzania imethibitisha tena dhamira yake ya kuunga mkono ukuaji endelevu wa masoko ya fedha ya Tanzania na kuchangia kwa maana katika maendeleo endelevu  ya uchumi wa taifa.

 

Hayo yalibainishwa na Rais wa chama hicho, Bw. Farid Yahya Ally, wakati wa hafla ya futari iliyofanyika Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Hafla hiyo ilijumuisha mjadala wa jopo kuhusu maendeleo na changamoto zinazoikabili sekta ya masoko ya fedha nchini Tanzania na iliwakutanisha wadau wa soko, watunga sera na wadhibiti wa sekta hiyo.

 

“Kupitia ushirikiano endelevu na wadhibiti, watunga sera pamoja na wadau wa sekta, chama kitaendelea kuunga mkono mipango inayolingana na malengo ya muda mrefu ya maendeleo ya Tanzania, ikiwemo azma ya Dira 2050 ambayo inalenga kujenga uchumi wa dola trilioni moja,” alisema Bw. Ally.

 

Akihutubia wawakilishi mashuhuri kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Soko la Hisa la Dar es Salaam, pamoja na Wakuu wa Masoko ya Kimataifa kutoka taasisi mbalimbali za kifedha, Bw. Ally alibainisha kuwa kama chombo cha kitaaluma kinachowakilisha wataalamu wa masoko ya fedha, ACI FMA Tanzania inatambua jukumu lake muhimu katika kuimarisha maendeleo na uadilifu wa masoko ya fedha nchini.

 

“Kuimarisha ushirikiano na watunga sera pamoja na wadhibiti ni sehemu muhimu ya dhamira yetu ya kukuza kanuni bora za uendeshaji wa soko na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa na mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa,” alisema.

 

Hafla ya futari ilikuwa jukwaa muhimu la majadiliano na ushirikiano kati ya washiriki wa soko, watunga sera na wadhibiti. Majadiliano yalilenga kutafuta njia za kuziba mapengo ya kitaasisi yaliyopo na kuimarisha ushirikiano katika kujenga mazingira imara na yenye ustahimilivu kwa masoko ya fedha.

 

Wakati wa majadiliano hayo, washiriki walibainisha changamoto kadhaa zinazoathiri sekta ya masoko ya fedha, ikiwemo ukosefu wa utofauti wa bidhaa za kifedha, taratibu ngumu za udhibiti kwa washiriki wapya wa soko, pamoja na utegemezi mkubwa wa ufadhili unaotolewa na taasisi za kifedha.

 

Akijibu hoja hizo, Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Bw. Peter Nalitolela, alikiri kuwa ingawa masoko ya mitaji nchini Tanzania yanaendelea kukua, uelewa wa wawekezaji wadogo kuhusu soko hilo bado ni mdogo.

 

Alisema kuwa licha ya idadi ya akaunti za Central Depository System (CDS) kuwa ndogo kwa kiasi, hivi karibuni soko limeanza kushuhudia ongezeko la wawekezaji wapya wanaoingia kwenye soko la hisa.

 

“Ingawa wawekezaji wengi zaidi wanaonesha nia ya kuingia sokoni, changamoto kadhaa bado zinaendelea kuwepo, ikiwemo ukosefu wa utofauti wa bidhaa za kifedha na maandalizi ya soko kukidhi ongezeko la ushiriki wa wawekezaji,” alisema.

 

Bw. Nalitolela pia alibainisha kuwa mauzo ya awali ya hisa kwa umma (IPOs) yamepungua si Tanzania pekee bali pia kimataifa, hali inayoakisi mwenendo mpana wa masoko duniani.

 

Hata hivyo, alisisitiza kuwa Tanzania inaendelea kubadilika taratibu kutoka katika mfumo wa uchumi unaoongozwa zaidi na serikali kuelekea uchumi unaochochewa zaidi na sekta binafsi, hatua ambayo tayari imeanza kuleta mwamko chanya katika masoko ya mitaji na hisa.

 

Wakati huohuo, Rais wa ACI FMA Duniani, Bw. Rui Correia, alitangaza kuwa chama hicho kitaanzisha mpango wa ufadhili wa masomo kwa wanawake barani Afrika ili kusaidia wataalamu wanawake katika sekta ya masoko ya fedha.

 

“Hili ni jambo tunalotaka kufanya hasa tunapokaribia Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani. Kwa mwaka huu tutazingatia ufadhili wa masomo kwa wanawake barani Afrika, na mwaka ujao tutaanzisha mpango mwingine,” alisema Bw. Correia.

 

Alisisitiza kuwa chama hicho kinathamini sana ushirikishwaji wa maarifa na maendeleo ya kitaaluma ndani ya jamii ya wataalamu wa masoko ya fedha.

 

“Kwetu sisi, elimu si kupata vyeti pekee. Ni kuhusu kubadilishana utaalamu, maarifa na uzoefu katika nyanja mbalimbali za masoko ya fedha,” aliongeza.

 

ACI FMA Tanzania ni shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi chini ya mwavuli wa ACI FMA Global. Chama hicho kinakuza kanuni bora za uendeshaji wa soko kwa kuwapatia wataalamu wa masoko ya fedha mafunzo, fursa za kushiriki katika shughuli za kitaaluma pamoja na vyeti vinavyotambulika kimataifa.

Ofisa Mtendaji  Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Bw. Peter Nalitolela (kulia), Rais wa ACI FMA Global Bw. Rui Correia, na Rais wa ACI FMA Tanzania Bw. Farid Yahya Ally wakichukua chakula cha futari katika hafla iliyoandaliwa na ACI FMA Tanzania jijini Dar es Salaam jana. Hafla hiyo iliwakutanisha wadau wa masoko ya fedha, watunga sera na wadhibiti ili kuimarisha ushirikiano na kukuza mazingira imara ya masoko ya fedha nchini.
Rais wa ACI FMA Tanzania, Bw. Farid Yahya Ally, akizungumza na washiriki wakati wa hafla ya futari, iliyofanyika Dar es Salaam jana. Hafla hiyo iliwakutanisha wadau wa masoko ya fedha, watunga sera na wadhibiti ili kuimarisha ushirikiano na kukuza mazingira imara ya masoko ya fedha nchini.
Rais wa ACI FMA Tanzania Bw. Farid Yahya Ally (kulia) akibadilishana mawazo na Rais wa ACI FMA Duniani, Bw. Rui Correia (kushoto) pamoja na Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Stanslaus Shenyali, wakati wa hafla ya futari, iliyoandaliwa na ACI FMA Tanzania Dar es Salaam jana.
Ofisa Mtendaj  Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam Bw. Peter Nalitolela (kulia) akizungumza wakati wa mjadala uliofanyika pamoja futari iliyoandaliwa na ACI FMA Tanzania jijini Dar es Salaam jana. Hafla hiyo iliwakutanisha wadau wa masoko ya fedha, watunga sera na wadhibiti ili kuimarisha ushirikiano na kukuza mazingira imara ya masoko ya fedha nchini.
Baadhi ya wageni waalikwa wakiwa katika  hafla ya futari iliyoandaliwa na ACI FMA Tanzania, jijini  Dar es Salaam jana. Hafla hiyo iliwakutanisha wadau wa masoko ya fedha, watunga sera na wadhibiti ili kuimarisha ushirikiano na kukuza mazingira imara ya masoko ya fedha nchini.
Rais wa ACI FMA Tanzania Bw. Farid Yahya Ally (wa nane kutoka kushoto), Rais wa ACI FMA Duniani, Bw. Rui Correia (wa sita kutoka kushoto), maofisa wa ACI na wageni wengine waalikwa wakipiga picha ya pamoja baada ya hafla ya futari iliyofanyika Dar es Salaam jana. Hafla hiyo iliwakutanisha wadau wa masoko ya fedha, watunga sera na wadhibiti ili kuimarisha ushirikiano na kukuza mazingira imara ya masoko ya fedha nchini.


Post a Comment

0 Comments