About Me

header ads

Absa Group Yatangaza Mabadiliko Muhimu ya Uongozi wa Juu

 

Absa Group imetangaza mabadiliko kadhaa ya kimkakati katika safu yake ya uongozi wa juu, kufuatia kukamilika kwa Mkakati wake ulioboreshwa wa Grupu wa Umajumui wa Afrika (Pan-Afrika). Hatua hiyo inalenga kuimarisha uwezo wa kimkakati, kukuza ukuaji unaoongozwa na mteja, kuimarisha misingi ya utawala bora, pamoja na kuendeleza mipango madhubuti ya urithishaji wa uongozi ndani ya taasisi hiyo.

 Sitoyo Lopokoiyit Ateuliwa Kuongoza Benki ya Wateja Binafsi na Wateja Maalum 

Sitoyo Lopokoiyit ameteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi na Wateja Maalum, kuanzia tarehe 1 Aprili 2026. Lopokoiyit ni kiongozi mwenye uzoefu mkubwa katika sekta ya huduma za kifedha na mawasiliano, akiwa na utaalamu wa kina katika ubunifu wa huduma za kifedha za kidijitali, thamani kwa wateja na mabadiliko makubwa ya biashara.

Kabla ya uteuzi huu, alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa M-PESA Africa na Afisa Mkuu wa Huduma za Kifedha katika Safaricom, ambako aliongoza mkakati na ukuaji wa jukwaa kubwa zaidi la fintech barani Afrika. Akiwa na zaidi ya miaka 12 ya uzoefu katika fintech, amechangia kwa kiasi kikubwa kupanua huduma za M-PESA hadi kuhudumia zaidi ya wateja milioni 56 na zaidi ya biashara milioni 5 barani Afrika.

Katika kipindi chake Safaricom tangu mwaka 2011, Lopokoiyit alishika nyadhifa mbalimbali za juu ikiwemo Mkuu wa Mkakati na Maendeleo ya Biashara wa M-PESA, pamoja na kuongoza shughuli za kampuni nchini Tanzania. Ameongoza uzinduzi wa ubunifu kama vile M-PESA Super App na Fuliza, na kuanzisha ushirikiano wa kimkakati na majukwaa ya kimataifa kama PayPal na Alipay.

Akizungumza kuhusu uteuzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Absa Group, Kenny Fihla, alisema:

“Uteuzi huu unaonesha msisitizo wa kimkakati wa Absa katika kutoa suluhisho jumuishi na linalomweka mteja mbele katika huduma zetu za Benki ya Wateja Binafsi na Wateja Maalum, huku tukifungua fursa mpya za ukuaji.”

 Prabashni Naidoo Ateuliwa Afisa Mkuu wa Utawala 

Prabashni Naidoo, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Ukaguzi wa Ndani wa Kundi, atachukua nafasi mpya iliyoundwa upya ya Afisa Mkuu wa Utawala wa Kundi (Group Chief Governance Officer), kuanzia tarehe 1 Machi 2026. Nafasi hiyo itajumuisha Idara za Sheria, Uzingatiaji wa Sheria (Compliance) na Sekretarieti ya Abs Group..

Naidoo anatambuliwa kama mtaalamu mwenye heshima kubwa katika masuala ya utawala bora, akiwa na uzoefu mpana katika ukaguzi, usimamizi wa viashiria vya hatari, mahusiano ya kisheria na udhibiti, pamoja na uhakiki wa taasisi.

 Rushdi Solomons Apandishwa Cheo Kuongoza Ukaguzi wa Ndani 

Rushdi Solomons amepandishwa cheo kuwa Afisa Mkuu wa Ukaguzi wa Ndani wa Kundi (Group Chief Internal Audit Officer), kuanzia tarehe 1 Machi 2026. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mtendaji Mkuu: Mkakati wa Uzingatiaji, Mahusiano ya Udhibiti na Utawala.

Solomons ana uzoefu mkubwa katika sekta za umma na binafsi, akiwa amewahi kushika nyadhifa katika Deloitte, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Afrika Kusini, pamoja na PwC.

 Fatima Newman Ateuliwa Afisa Mkuu wa Masuala ya Sheria 

Fatima Newman ameteuliwa kuwa Afisa Mkuu wa Masuala ya Sheria (Chief Compliance Officer), kuanzia tarehe 1 Machi 2026. Fatima ana uzoefu wa miaka 28 katika sekta mbalimbali, akiwa na utaalamu katika usimamizi wa hatari, uzingatiaji wa sheria, masuala ya udhibiti na utawala.

Amehudumu katika nyadhifa za juu katika EOH Group Limited, pamoja na MTN South Africa, na pia ndani ya Absa.

Akizungumzia mabadiliko hayo, Fihla aliongeza:

“Uteuzi huu unaakisi kina cha vipaji vilivyopo ndani ya Absa pamoja na uimara wa mipango yetu ya urithishaji wa uongozi. Tunaendelea kujenga timu ya uongozi iliyo tayari kwa siku zijazo, tukihakikisha tuna uwezo sahihi wa kutekeleza malengo yetu ya kimkakati na kuimarisha mfumo thabiti wa utawala bora.”

Post a Comment

0 Comments