About Me

header ads

Benki ya Absa Tanzania na ASA Microfinance Yaadhimisha Miaka Minne ya Mafanikio katika Kuwawezesha Wanawake na Kubadilisha Jamii

 



Benki ya Absa Tanzania, kwa ushirikiano na taasisi inayotoa huduma za kifedha ya ASA Microfinance, inajivunia kuadhimisha mwaka wa nne wa ushirikiano wa kipekee ambao umewezesha zaidi ya wanawake wajasiriamali 50,000 nchini Tanzania kupata mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 40 za Kitanzania.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2022, ushirikiano huu wa muda mrefu umeenda zaidi ya kutoa mikopo pekee, kila mwanamke mjasiriamali aliyewezeshwa si tu anabadilisha maisha yake binafsi, bali pia anagusa maisha ya familia yake, wafanyakazi, wasambazaji, na jamii pana inayomzunguka. Utafiti wa maendeleo unaonyesha kwamba kumwezesha mjasiriamali mmoja mwanamke nchini Tanzania kunaweza kuinua maisha ya watu 15 hadi 20 walioko karibu naye, hii inamaanisha kwamba ushirikiano kati ya Benki ya Absa na ASA Microfinance umegusa maisha ya karibu watanzania milioni moja, ukiimarisha familia na kuchochea ukuaji jumuishi wa kiuchumi.

Akizungumza kuhusu mafanikio haya jijini Dar es Salaam leo katika mkutano na waandishi wa habari, Obedi Laiser, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, alisema: “Taasisi nyingi huzingatia uwezeshaji wa wanawake kama mradi wa muda mfupi, kwa Absa, hili ni jukumu lenye kusukumwa na dhamira ya kweli. Kwa kuwawezesha zaidi ya wanawake 50,000 kupata mitaji na kukuza biashara zao, tunaona athari chanya zinazopanuka, zinazobadilisha familia, kuelimisha watoto, kuunda ajira, na kujenga ustahimilivu katika jamii. Hivi ndivyo tunavyoishi kauli mbiu yetu ya Kuiwezesha Afrika ya kesho, pamoja… hatua moja baada ya nyingine, kwa sababu kwetu Absa, Stori yako ina thamani.”

Kwa upande wake, Muhammad Shah Newaj, Ofisa Mtendaji kuu wa ASA Microfinance Tanzania, aliongeza:
“Ushirikiano wetu na Benki ya Absa Tanzania umeleta mageuzi makubwa. Kupitia msaada wa Absa, ASA imeweza kupanua huduma za mikopo midogo kwa maelfu ya wanawake wajasiriamali ambao wangeachwa nje ya mfumo rasmi wa kifedha. Pamoja, hatufadhili biashara pekee , tunafadhili heshima, matumaini, na fursa zinazoinua vizazi.”

Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, ushirikiano huu umeunganisha utoaji wa mitaji na mafunzo ya elimu ya kifedha, kuhakikisha kwamba wanawake wajasiriamali hawapati mikopo tu bali pia maarifa ya kuiendesha kwa uendelevu. Mapema mwezi huu, wanawake 50 kutoka Dar es Salaam walishiriki katika programu ya elimu ya kifedha iliyojumuisha mada za upangaji bajeti, akiba, uwekezaji, na utunzaji wa kumbukumbu, hatua muhimu katika kubadilisha mikopo kuwa uwezeshaji endelevu wa kiuchumi.

Mpango huu unaonyesha mkakati wa Uwajibikaji wa Kijamii wa Absa, unaolenga ujumuishaji wa kifedha, ujasiriamali, na maendeleo endelevu. Pia unaendana na ajenda ya kitaifa ya ujumuishaji wa kifedha nchini Tanzania kwa kupanua huduma za mikopo na elimu kwa makundi yasiyohudumiwa ipasavyo, hivyo kuleta mabadiliko ya kudumu ya ustahimilivu wa kiuchumi.

Kupitia ushirikiano huu endelevu, Benki ya Absa Tanzania na ASA Microfinance zinaendelea kuandika simulizi za mabadiliko , simulizi ambazo mwanamke mmoja aliyewezeshwa hubadilisha si maisha yake tu, bali pia maisha ya wengi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser (Katikati), akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, wakati akitangaza mafanikio ya ushirikiano wa kibiashara kati ya benki hiyo na taasisi inayotoa huduma za kifedha ya ASA Microfinance kwa kipindi cha miaka minne. Kupitia ushirikiano huo, Benki ya Absa imeikopesha ASA kiasi cha shs billioni 40 zilizoiwezesha taasisi hiyo kutoa mikopo kwa wanawake wajasiriamali zaidi ya 50,000 kutoka sehemu mbalimbali nchini Tanzania.  Wengine kutoka kushoto ni, Meneja Huduma za Jamii na Matukio wa Benki ya Absa, Bi. Abigail Lukuvi, Mkurugenzi wa wateja wa Makampuni wa Absa, Nellyana Mmanyi, Ofisa Mtendaji Mkuu wa ASA Microfinance Tanzania, Bw. Muhammad Shah Newaj na Meneja Mahusiano ya Jamii na Utawala wa ASA, Bi. Veneranda Francis.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser (wa tatu kushoto), akikabidhi tuzo kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi inayotoa huduma za kifedha ya ASA Microfinance Tanzania, Bw. Muhammad Shah Newaj, kwa kutambua mchango wa taasisi hiyo, katika kuwawezesha wanawake wajasiriamali nchini, kwa kupitia masuluhisho mbalimbali ya kifedha. Ilikuwa ni katika hafla ambayo Absa ilitangaza mafanikio ya ushirikiano wa kibiashara kati ya benki na taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka minne. Kupitia ushirikiano huo, Benki ya Absa imeikopesha ASA kiasi cha shs billioni 40 zilizoiwezesha taasisi hiyo kutoa mikopo kwa wanawake wajasiriamali zaidi ya 50,000 kutoka sehemu mbalimbali nchini Tanzania.  Wengine kutoka kushoto ni, Meneja Huduma za Jamii na Matukio wa Benki ya Absa, Bi. Abigail Lukuvi, Mkurugenzi wa wateja wa Makampuni wa Absa, Bi. Nellyana Mmanyi, na Meneja Mahusiano ya Jamii na Utawala wa ASA Microfinance, Bi. Veneranda Francis.
Meneja Huduma za Jamii na Matukio wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Abigal Lukuvi (kushoto), akizungumza katika hafla ambayo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Obedi Laiser (wa tatu kushoto), akitangaza mafanikio ya ushirikiano wa kibiashara kati ya benki hiyo na taasisi inayotoa huduma za kifedha ya ASA Microfinance kwa kipindi cha miaka minne. Kupitia ushirikiano huo, Benki ya Absa imeikopesha ASA kiasi cha shs billioni 40 zilizoiwezesha taasisi hiyo kutoa mikopo kwa wanawake wajasiriamali zaidi ya 50,000 kutoka sehemu mbalimbali nchini Tanzania.  Wengine kutoka kushoto kwake ni, Mkurugenzi wa wateja wa Makampuni, Bi. Nellyana Mmanyi, Ofisa Mtendaji Mkuu wa ASA Microfinance Tanzania, Bw. Muhammad Shah na Meneja Mahusiano ya Jamii na Utawala wa ASA, Bi. Veneranda Francis.

Post a Comment

0 Comments