Katika juhudi za kuimarisha afya kwa wote, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na shirika la Amref Tanzania wamefanya majadiliano ya pamoja ili kuboresha utoaji wa huduma za kibingwa bobezi kwa jamii kupitia huduma mkoba.
Akizungumza katika Kikao hicho kilichofanyika leo Julai 22, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji MNH Dkt. Delilah Kimambo amewashukuru Amref kwa kuendela kuwa na mchango mkubwa kwenye kusaidia Huduma Mkoba Nchini kwa kushirikia na Madaktari Bingwa na Bobezi kutoka hospitalini hapo kwa kipindi kirefu huku akiwahakikishia ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha huduma bora za kibingwa zinawafikia wananchi katika maeneo yao kwa wakati.
“Niwashukuru na niwahakikishie ushirikiano wa kutosha na sisi tupo tayari kuendelea kushirikiana kutoa huduma mkoba [outreach] kuwafikia wananchi popote walipo,lakini pia tunatakiwa kuingia ndani zaidi kujua changamoto kubwa za uzazi zinazowakumba kina mama kwenye huduma za Afya za Awali,kuwaongezea ujuzi wataalamu vituo vya Afya na kuongezea ujuzi” ameeleza Dkt. Kimambo.
Aidha kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Amref Tanzania Bw. Anthony Chamungwana amempongeza Dkt, Kimambo kwa kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji MNH na kuahidi kuendeleza mahusiano na ushirikiano uliopo.
Kulingana na takwimu za miaka minne iliyopita MNH na Amref wamefanikiwa kuwafikia wananchi zaidi ya 4,000 kutoka mikoa mbali mbali nchini huku zaidi ya 5,00 walifanyiwa upasuaji kupitia huduma mkoba.
0 Comments