Na Mwamvua Mwinyi, Pwani Disemba 17,2024
Kiwanda kipya cha kuzalisha malighafi za kutengeneza mabati (coils )Kinglion kilichojengwa katika eneo la viwanda Zegereni kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 35,000.
Meneja wa Kampuni ya Kinglion, Arnold Lyimo, amesema alieleza kuwa kiwanda hicho kitaleta ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira za muda zaidi ya 5,000, hatua ambayo itaongeza mchango wa kampuni hiyo katika ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Pwani na taifa kwa ujumla.
Wakati wa maonyesho ya nne ya biashara na uwekezaji yanayofanyika Mailmoja, Kibaha, Lyimo alisema maonyesho hayo ni fursa muhimu kwao kuonyesha bidhaa wanazozalisha na kujifunza mahitaji ya soko.
Alifafanua kiwanda hicho kimejengwa na kinatarajia kuanza uzalishaji mwishoni mwa mwaka huu.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, alitembelea banda la kampuni hiyo na kuipongeza kwa ubora wa bidhaa wanazozalisha, huku akisisitiza umuhimu wa uzalishaji wa bidhaa zenye viwango vya juu ili ziweze kushindana sokoni.
Akizindua maonyesho hayo, Dk. Jafo alisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji, hali itakayochochea uzalishaji wa bidhaa bora na endelevu.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani aliishukuru Kampuni ya Kinglion kwa kuwa mdhamini wa maonyesho hayo, akiahidi kushughulikia changamoto ya barabara km 2.5 katika eneo lao la uwekezaji ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora muda wote.
0 Comments