About Me

header ads

BILIONI SABA KUMTUA MAMA NDOO KICHWANI WILAYANI MAFIA

 

Na Mwamvua Mwinyi,Mafia Novemba 21, 2024

Serikali imewekeza zaidi ya sh. bilioni saba katika miradi ya maji wilayani Mafia, miradi ambayo inatekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA ili kupunguza kero ya ukosefu wa maji safi na salama, hasa kwa lengo la kumtua mama ndoo kichwani. 


Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo, alisema miradi hiyo inalenga kuimarisha maisha ya wananchi kwa kuhakikisha huduma ya maji inawafikia kwa urahisi.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua miradi hiyo katika kata za Kilindoni na Kiegeani, Mangosongo alibainisha kuwa juhudi hizi zinaendana na maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

"Lengo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kumtua mama ndoo kichwani haliwezi kufikiwa kama miradi hii haitasambazwa ipasavyo na kuwafikia wananchi wote," Mangosongo.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ametoa rai kwa wasimamizi wa miradi kuhakikisha wananchi wanashirikishwa kikamilifu katika kila hatua ya utekelezaji, huku akiwapongeza wananchi wanaojitolea ardhi kwa ajili ya miradi hiyo.

Meneja wa RUWASA wilayani Mafia, Mhandisi Clement Lyoto, anaahidi kukamilisha miradi yote kwa wakati na kuhakikisha inatoa matokeo chanya.

Aliwataka wananchi kushirikiana na wakala huo kwa kulinda na kutunza miundombinu ya miradi hiyo.

"Ni jukumu letu kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati, lakini pia tunahitaji ushirikiano wa jamii katika kuilinda ili idumu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo," alisema Mhandisi Lyoto.
Wananchi waliohudhuria kwenye ukaguzi wa miradi hiyo waliishukuru serikali kwa juhudi kubwa za kufikisha huduma ya maji karibu na makazi yao. 

Ahmad Bakari, mkazi wa kitongoji cha Kitundu katika kijiji cha Dongo, alieleza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaboresha maisha yao, hasa kwa wakulima.

"Mradi huu sisi wananchi tunautaka ,ukikamilika, maisha yetu yatabadilika kwa kiasi kikubwa, hasa kwa sisi tunaofanya kilimo," alisema Bakari.

Miradi inayotekelezwa na RUWASA wilayani Mafia inajumuisha ujenzi wa matenki makubwa ya maji, visima, na ofisi za usimamizi wa maji. 



 

Post a Comment

0 Comments