MKUU wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva amekimwagia sifa Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao kwa kuguswa na mambo ya kijamii,huku akiwaomba kuzidi kuwa walezi wazuri kwa vyama vya msingi viweze kufikia malengo jadidi ya kuwahudumia wakulima.
Katika kutekeleza msingi wa saba wa ushirika wa kuisaidia jamii, Lindi Mwambao kimemkabidhi Mkuu wa Wilaya hiyo, Mwanziva madawati 150, viti mwendo viwili na mataili manne kwaajili ya jeshi la Polisi, vyote vikiwa na thamani ya Sh. 19,700,000.
Hafla ya makabidhiano ya msaada huo imefanyika leo Novemba 20, 2024 katika Ofisi za chama hicho zilizopo mtaa wa Mmongo- Mitwero, Kata ya Rasibula na kuhudhuriwa na makundi mbalimbali ya watu wakiwemo wakulima na wanafunzi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya ya Lindi, Mwanziva licha ya kuipongeza bodi ya chama kikuu hicho kwa msaada huo, ametumia fursa hiyo kuwaomba kuzidi kuwa walezi wazuri wa vyama vya msingi na kuifikia jamii kama msingi wa saba wa ushirika unavyotaka, huku wakiendelea kutoa huduma bora kwa wakulima kwa kuhakikisha wanatoa taarifa kwa viongozi endapo kutatokea changamoto ili zipatiwe ufumbuzi wa haraka.
‘’Mmeigusa jamii kwa kutoa madawati 150 ambayo yanakwenda kuunga mkono jitihada za Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu, lakini mmewagusa wenye mahitaji kwa kuwapa viti mwendo, jeshi la polisi hamjaliacha linalofanya kazi kubwa ya kutunza amani mmewapa mataili, neno letu kubwa ni asanteni sana,’’ alisema Mwanziva.
Aidha, kuhusu msimu wa mauzo ya korosho kwa mwaka 2024/2025 amesema wakulima wamepata bei nzuri kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika sekta ya kilimo nchini ambapo viuatilifu vimetolewa bure pamoja na kuboreshwa kwa huduma za ugani ili kuwagusa wakulima kukuza na kuongeza uzalishaji.
‘’Tumeona kupitia mfumo wa mauzo wa bidhaa wa Tmx kwenye mnada wa kwanza uliofanyika Mtama bei ya kilo moja ya korosho ghafi ilifika Sh. 3860 na mkoa wa jirani ilifika zaidi ya Sh. 4000, hizi ni bei nzuri na kwa taarifa tulizonazo kutoka Bodi ya Korosho hadi sasa kiasi cha Sh. Trilioni 1 imekwenda kwa wakulima zikilipwa kwa uwazi na tunawashukuru Amcos zote na tunaomba tuendelee kuwahudumia vizuri wakulima kwani wao ndio chanzo cha haya yote tunayoyazungumza."
Awali, Meneja wa Lindi Mwambao, Nurdin Said Swallah amesema wamezidi kusukumwa kwa namna Rais Dkt. Samia anavyojali ushirika kwa kusambaza pembejeo bure kwa wakulima hali iliyosaidia kuongeza uzalishaji wa korosho, lakini ametoa kiasi cha Sh.Bilioni 5 kwaajili ya uanzishwaji wa benki ya ushirika hivyo wanaushirika wameamua kumuunga mkono kwa kutoa madawati yatakayokwenda kuwasaidia wanafunzi kupata elimu wakiwa katika mazingira mzuri.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Elimu Msingi kutoka Manispaa ya Lindi, Mwalimu Alex Mkwango ameeleza kufurahishwa na msaada huo akisema licha ya kuwepo kwa mikakati ya kupunguza upungufu wa madawati, wanaamini msaada huo utakwenda kupunguza uhaba wa madawati katika manispaa hiyo ambapo kwa sasa kuna mahitaji ya madawati 10913, yaliyopo ni 8921 na hivyo kufanya upungufu wa madawati 1272.
0 Comments