Na Albano Midelo
Bandari ndogo ya Liuli mwambao wa ziwa Nyasa wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, inajulikana hasa kutokana hospitali ya Mtakatifu Anna ya kanisa Anglikana inayohudumia wagonjwa wengi katika wilaya Nyasa.
Katika sekta ya utalii bandari ya Liuli ni eneo lenye utajiri wa vivutio vya utalii wa aina mbalimbali. Jina Liuli lina maana ya 'jiwe lile'. Wakati wa ukoloni wa Kijerumani Liuli iliitwa "SPHINXHAFEN" yaani bandari ya SFINKSI kwa sababu ya kuwepo utajiri wa miamba mikubwa inayofanana na sanamu mashuhuri kwenye Piramidi za giza kama nchini Misri.
Tarehe 13/8/1914 mwanzoni mwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia Waingereza walishambulia katika eneo la Liuli meli ya pekee ya Wajerumani kwenye ziwa Nyasa ambapo katika Jiwe kubwa la Pomonda lililopo meta 300 ndani ya ziwa Nyasa lilitumika kama maficho ya askari wakati wa vita.
Kwa mujibu wa habari katika gazeti la Times iliyochapishwa mwaka 1914, Uingereza iliwahi kuingia katika vita ya kwanza ya Dunia Agosti 4,1914 na kwamba Siku chache baadaye Nahodha Mwingereza Edmund Rhoades katika kisiwa cha Nkhata Bay nchini Malawi alipokea amri ya kuzamisha meli Hermann von Wissmann iliyokuwa meli pekee ya Wajerumani kwenye ziwa Nyasa.
Meli hii ilikuwa chini ya Nahodha wa kijerumani aliyeitwa Berndt ambapo baada ya kupata amri, Rhoades aliendesha meli yake HMS Gwendolyn kuelekea Sphinxhafen (Liuli) kwa sababu alijua meli ilikuwa wapi. Manahodha wote wawili walikuwa marafiki waliowahi kutembeleana mara kwa mara na kukaa pamoja.
HMS Gwendolyn ilipokaribia bandari ya Liuli, Mpiganaji mzinga wa pekee wa meli na mfanyabiashara mmoja Mskoti alikuwa mtu wa pekee mwenye kujua matumizi ya mzinga hivyo alianza kufyatulia risasi dhidi ya Hermann von Wissmann.
Dakika chache baadaye boti ndogo ilikaribia haraka HMS Gwendolyn. Nahodha Berndt akapanda meli na kumwuliza mwenzake kwa hasira, kwa nini amelewa wakati wa mchana.
Hakujua kuwa vita ilianza tayari katika bara la Ulaya hivyo Rhoades alimtangaza Nahodha wa kijerumani kuwa mfungwa wa vita.
Habari ya ushindi huo ilipelekwa London kwa simu na tarehe 16 Agosti mwaka 1914,gazeti la Times lilichapisha na kutangaza ushindi wa Uingereza katika bandari ya Liuli ziwa Nyasa "Naval victory on Lake Nyasa".
Wakati ule Waingereza waliondoa mzinga mdogo wa meli na vipuli kadhaa ili meli isitumike tena bila kuiharibu. Mwaka 1915 Wajerumani walikuwa wameleta tena vipuli na kutengeneza meli ambapo Waingereza walirudi Liuli na kuzamisha meli ya Hermann von Wissmann katika bandari ya Liuli.
Baada ya vita meli ilifufuliwa tena na kufanya kazi kwa Waingereza ambapo hadi sasa maboya yamewekwa katika eneo la Liuli kuonesha mahali meli hiyo ilipozamishwa.
0 Comments