About Me

header ads

WANANCHI BAGAMOYO WAPOKEA ELIMU YA FEDHA

 

Na. Saidina Msangi, WF, Bagamoyo, Pwani.

Watumishi na wananchi wa wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, wameishukuru Serikali kwa kuwapa mafunzo ya elimu ya fedha yanayotolewa na Wizara ya Fedha kwa kuwa yamewafungua na kuwapa mwanga wa kujiandaa kustaafu wakiwa na uchumi imara.

Walitoa shukrani hizo kwa nyakati tofauti Mjini Bagamoyo, mkoani Pwani, baada ya mafunzo ya siku mbili yaliyotolewa na Maafisa kutoka Wizara ya Fedha ukihusisha watumishi katika ukumbi wa mikutano wa wilaya, na wananchi katika ukumbi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, (TaSUBa).

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Bagamoyo, Bi. Zuwena Ungele, alisema kuwa elimu ya fedha waliyoipata imewapa motisha ya kuanza kujiandaa na maisha ya kustaafu.

‘’Sisi ni mabalozi wa watumishi wa Serikali kwa ujumla sasa unapostaafu ukawa na maisha mabaya unaleta picha mbaya kuwa unaweza kuwa mtumishi wa Serikali unastaafu ukiwa umechoka kimaisha hivyo tujipange kulinda taswira ya Serikali kwa kujiandaa kustaafu tukiwa imara kiuchumi’’, alisema Bi. Ungele.

Alisisitiza kuwa watumishi ni wastaafu watarajiwa hivyo ni vema kuanza kuweka mpango na maandalizi ya kustaafu mapema ili wakati ukifika wawe na akiba ya kuwawezesha kuishi Maisha yenye hadhi.

Aidha, wameishukuru Wizara kwa elimu ya fedha na kutoa rai kuwa elimu hiyo itolewe mara kwa mara ili iwe chachu ya kuhamasisha watumishi na wananchi kwa ujumla kujenga utaratibu wa kujiandaa na maisha ya kustaafu.

Akizungumza wakati akitoa elimu kwa watumishi na wananchi wa Wilaya ya Bagamoyo, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya alisema kuwa Serikali inatekeleza programu ya utoaji wa elimu ya fedha kwa wananchi ili kuhakikisha kuwa wanapata elimu ya fedha ya kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi kuhusu fedha zao.

‘‘Ni lazima kuwa makini sana katika kupanga matumizi ya fedha, hakikisha unasimamia mapato na matumizi, matumizi yasizidi mapato, kila fedha unayopata tunza asilimia kumi tuwe na utaratibu wa kuweka akiba katika sehemu rasmi kwani akiba haiozi na kuhakikisha kuwa unapochukua mikopo taasisi hiyo imesajiliwa na ina leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania,’’ alisisitiza Bw. Kibakaya.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, akisikiliza maelezo kuhusu elimu ya fedha wakati akipokea kipeperushi chenye taarifa za elimu ya fedha kutoka kwa Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, wakati Maafisa wa Wizara ya Fedha walipowasili kwa lengo la kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, Bi. Zuwena Ungele, akizungumza wakati akiwakaribisha Maafisa wa Wizara ya Fedha walipofika kutoa elimu ya fedha kwa watumishi wa Wilaya ya Bagamoyo katika ukumbi wa mikutano wa wilaya hiyo. Kulia ni Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, na kushoto ni Afisa Usimamizi wa Fedha Mwandamizi wa Wizara ya Fedha, Bi. Mary Mihigo.
Afisa Masoko na Uhusiano Mwandamizi wa Mfuko wa Uwekezaji wa UTT AMIS, Bw. Rahim Mwanga, akitoa elimu ya uwekezaji, hususan mifuko ya uwekezaji inayopatikana katika Mfuko wa Uwekezaji wa UTT Amis na jinsi wanavyoweza kunufaika na fursa za uwekezaji, wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha iliyotolewa na Maafisa kutoka Wizara ya Fedha, kwa watumishi wa Wilaya ya Bagamoyo katika ukumbi wa mikutano wa Wilaya ya Bagamoyo, Pwani.
Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha Bw. Stanley Kibakaya, akitoa elimu ya fedha kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia taasisi za fedha zilizosajiliwa wanapochukua mikopo ili kuwawezesha kuondokana na mikopo umiza pamoja na umuhimu wa kuzingatia mapato na matumizi ili wajiwekee akiba, wakati Maafisa wa Wizara ya Fedha walipokuwa wakitoa elimu ya fedha kwa wananchi katika ukumbi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, (TaSUBa), Bagamoyo, Pwani.



Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Bagamoyo wakisoma vipeperushi walivyopewa na Maafisa kutoka Wizara ya Fedha waliowasili kutoa elimu ya fedha kwa watumishi, kuhusiana na usimamizi wa fedha binafsi, dhamana za mikopo, riba pamoja na uwekezaji, katika ukumbi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, (TaSUBa), Bagamoyo, Pwani.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Bagamoyo -Pwani)


Post a Comment

0 Comments