Mstahiki Meya Songoro aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, katika Shule ya Msingi Msisiri B, wakati akipokea msaada wa madawati 30 yalitolewa na DCB kwa ajili ya shule hiyo, huku madawati yaliyosalia yakitarajiwa kupelekwa katika shule zenye uhitaji mkoani humo.
“Benki ya DCB mmeishika mkono serikali, tunawashukuru sana, serikali haiwezi kufanya kila kitu, ushirikiano kutoka kwa wadau ni jambo muhimu, leo benki hii imeanza, natoa wito kwa wadau wengine wajitokeze kuwekeza katika elimu ya watoto wetu ili tuweze kuwa na Taifa bora la baadae.
“Manispaa ilileta madawati 100, Mwananyama peke yake kila siku wanazaliwa watoto 100, hii ni Mwananyamala tu, bado maeneo mengine, maana yake kwa watoto wanaozaliwa sasa, baada ya miaka sita kutakuwa na mahitaji makubwa ya madawati, hivyo suala hili linapaswa kuwa endelevu”, alisema mstahiki meya.
Awali akizungumza kabla ya kukabidhi madawati hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DCB, Bw. Sabasaba Moshingi alisema msaada huyo unaenda sambasamba na makusudi halisi ya kuanzishwa kwa benki hiyo, miaka 22 iliyopita ikiwa ni kuinua maisha ya watanzania wenye kipato cha chini.
“Mwaka uliopita DCB tulitoa madawati 1000 katika shule mbalimbali na kwa mwaka huu tumedhamiria kutoa tena madawati 1000, Shule ya Msingi Msisiri B imebahatika kuwa ya kwanza, benki yetu itaendelea kushirikiana na serikali yetu katika kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza, hususan katika sekta ya elimu.
“Mbali na hili DCB itaendelea kuboresha huduma zake za kibenki ili ziweze kwenda sambamba na mahitaji halisi ya watanzania, huku tukiunga mkono juhudi za mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika jitahada zake za kuhakikisha huduma za kibenki zinawafikia watanzania wengi zaidi na katika kila kona ya nchi”, alisema Bw. Moshingi.
Benki ya Biashara ya DCB ilianzishwa mwaka 2002 na mwaka unaofuata kupewa leseni ya kujiendesha kama benki ya kijamii, ikijulikana kama Benki ya Watu wa Dar es Salaam ‘Dar es Salaam Community Bank’ ambayo wanahisa wake waanzilishi wakiwa ni Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na Manispaa zake za Ilala, Kinondoni na Temeke. Wanahisa wengine ni Mifuko ya NHIF na UTT AMIS pamoja na wananchi wa kawaida.
0 Comments