About Me

header ads

WATOA HUDUMA NDOGO ZA FEDHA TURIANI WATAKIWA KUFUATA SHERIA.

 

Na. Ramadhani Kissimba, WF, Morogoro


Watoa huduma ndogo za fedha katika tarafa ya Turiani Mkoani Morogoro wametakiwa kutoa huduma hizo kwa wananchi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa na serikali.

Akizungumza katika mfufulizo wa program ya kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya fedha, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mtibwa kaika tarafa ya Turiani, Wilayani Mvomero, Bi. Rudhaa Antony alisema baadhi ya Taasisi zilizopo katika tarafa hiyo zimekuwa zikitoa huduma bila ya kuzingatia taratibu zilizowekwa kwa kutoa huduma hizo kwenye magari badala ya kuwa na ofisi rasmi ya kutolea huduma hizo.

‘’Kwa kupitia elimu hii namuomba mwenyekiti wa wafanyabiashara aliyepo hapa, Taasisi za kutoa huduma ndogo za fedha zote zielezwe kuzingatia utozaji wa riba iliyowekwa na Benki Kuu, na pia kuacha kutoa huduma kwenye magari na kudai marejesho saa tisa usiku kwa sababu kufanya hivyo ni kinyume cha sheria’’ alisema Bi. Rudhaa.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa kutokana na elimu iliyotolewa itawasaidia wananchi wa tarafa ya Turiani hasa wakina mama kuachana na tabia ya kukopa kwenye Taasisi ambazo zimekuwa kero kwa wananchi jambo ambalo linachangia kuzorotesha Uchumi wa eneo hilo kutokana na wananchi kukimbia makazi yao kwa kushindwa kumudu kulipa madeni yanaoyotokana na riba kubwa inayotozwa na baadhi ya watoa huduma ndogo za fedha.

Aidha, Bi. Rudhaa aliwata Wananchi kuzifichua Taasisi zote zinazotoa huduma za fedha kwa kukiuka misingi ya leseni ya utoaji huduma hiyo hasa wale wanaotoa mikopo kandamizi (mikopo kausha damu) kwa wateja wake pamoja na kuwafanyia vitendo vya uzalilishaji ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya taasisi hizo.

Kwa upande wake, Mratibu wa huduma ndogo za fedha Wilaya ya Mvomero Bw. Clement Maganga alisema kuwa kwa sasa wananchi wameshaelewa mikopo inayokubalika kwa serikali inayotolewa na taasisi za fedha zilizosajiliwa ni ile isiyotoza riba zaidi ya asilimia 3.5 kwa mwezi na atakayezidisha kiwango hicho atakuwa amefanya kosa.

Bw. Maganga alisisitiza kuwa wananchi kuendelea kuimarisha na kusajili vikundi vyao vya huduma ndogo za fedha kwa sababu kuwepo kwa vikundi hivyo vitapunguza wimbi la wananchi wanaokimbilia katika mikopo ya kausha damu.

Aidha kwa upande wake, afisa usimamizi wa fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Jackson Mushumba alisema kuwa Taasisi zote zitakazo bainika kukiuka misingi ya utoaji mikopo kama ilivyoelekezwa na Benki Kuu ya Tanzania zitachukuliwa hatua ikiwemo kufutiwa leseni huku akiwataka wananchi kutoa taarifa kwa viongozi kuanzia ngazi ya Vijiji hadi Wilaya pindi wanaposhuhudia ukiukwaji wa misingi ya leseni kwa watoa huduma za fedha.

Bw. Mushumba aliongeza kuwa ili kuharakisha maendeleo kwa wananchi wa Wilaya ya Mvomero amewataka wananchi kuyaelewa masharti ya mikopo kabla ya kuchukua mikopo hiyo na kuzitaka taasisi zinazotoa huduma za fedha kuainisha na kuweka wazi masharti na taratibu za kupata mikopo katika taasisi zao.

Katika program ya utoaji elimu ya mauala ya fedha, Serikali inakusudia hadi kufikia mwaka 2025 takribani asilimia 80 ya wananchi wawe wamepata uelewa wa masuala ya fedha na kupelekea kundi kubwa kufaidika na huduma hizo na hivyo kuongeza fursa za kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi na hatimaye kuchangia katika kukuza pato la Taifa.Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mtibwa, katika tarafa ya Turiani , Wilayani Mvomero Bi. Rudhaa Antony akizungumza katika program maalum ya elimu kwa umma iliyofanyika katika katika ukumbi wa Community Centre uliopo kata ya Mtibwa Wilayani Mvomero.
Mkazi wa Mtibwa,Wilaya ya Mvomero Bi. Latifa Japhari akichangia mada iliyotolewa na wataalamu wa masuala ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na washirika wa sekta ya nchini katika program maalum ya elimu kwa umma iliyofanyika katika katika ukumbi wa Community Centre uliopo kata ya Mtibwa Wilayani Mvomero.
Mratibu wa huduma ndogo za fedha Wilaya ya Mvomero, Bw. Bw. Clement Maganga akizungumza wananchi wa kata ya Mtibwa, Tarafa ya Turiani Wilayani Mvomero waliohudhuria program maalum ya elimu kwa umma iliyofanyika katika katika ukumbi wa Community Centre uliopo kata ya Mtibwa Wilayani Mvomero.Mwenyekiti wa Umoja wa wafanyabiashara Wilaya ya Mvomero, Bw. Juma Kibacho akichangia jambo katika program maalum ya elimu kwa umma iliyofanyika katika katika ukumbi wa Community Centre uliopo kata ya Mtibwa Wilayani Mvomero.Afisa usimamizi wa fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Jackson Mushumba akizungumza wananchi wa kata ya Mtibwa, Tarafa ya Turiani Wilayani Mvomero waliohudhuria program maalum ya elimu kwa umma iliyofanyika katika katika ukumbi wa Community Centre uliopo kata ya Mtibwa Wilayani Mvomero. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha – Morogoro)

Post a Comment

0 Comments