About Me

header ads

Dkt. Biteko aipongeza Benki ya CRDB kuanzishwa kwa Benki ya Taifa ya Ushirika

 

Tabora. Tarehe 6 Julai 2024: Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameipongeza Benki ya CRDB kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuanzisha Benki ya Ushirika Tanzania ili itoe huduma kwa wanaushirika na wananchi wengine hivyo kuchangia zaidi katika uchumi.

Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Ipuli mjini Tabora ambako yeye alikuwa mgeni rasmi. 

“Benki ya CRDB mmetoa mchango mkubwa. Nawapongeza sana. Naamini benki hii mpya itasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto za mtaji wanazokabiliana nazo wakulima na wanaushirika kwa ujumla,” amesema Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Abdumajid Nsekela amesema mpaka sasa, TCDC yenye takribani miaka miwili tangu ilipoanza kutekeleza majukumu yake, imesimamia uanzishaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika na hatua zinazoendelea ni ufuatiliaji wa leseni kutoka BoT ili ianze kufanya kazi ndani ya mwaka huu.
“Tulijiwekea lengo la kukusanya shilingi bilioni 20 ili kuanzisha Benki ya Taifa ya Ushirika na mpaka sasa tuna zaidi ya shilingi bilioni 18 zinazotosha kukamilisha mchakato huu. Benki ya CRDB imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 10 kwenye mtaji huu,” amesema Nsekela akibainisha kuwa ushirika sasa unaendeshwa kidijitali kwani mpaka Juni 2024 vyama 6,361 vya ushirika vyenye wanachama 1,604,224 vilikuwa vinatumia mfumo huo.

Maboresho yaliyofanyika, Nsekela amesema yameviwezesha vyama vya ushirika kujiendesha kibiashara kwa kufufua viwanda na kujenga viwanda vipya ili kuongeza thamani ya mazao ya wakulima, kuhamasisha ushirika kwenye sekta mbalimbali na makundi maalum mfano mifugo, uvuvi na madini pamoja na kuimarisha uwekezaji wa mali za ushirika.

“Tume iliratibu utambuzi wa mali za vyama vikuu vya ushirika na SACCOS daraja B. Jumla ya mali za vyama vya ushirika 610 zenye thamani ya shilingi trilioni 4.2 zimetambuliwa,” amesema.
Akitoa salamu, Meneja wa Kanda ya Magharibi ya Benki ya CRDB, Jumanne Wagana amesema ili kufanikisha kuanzishwa kwa Benki ya Taifa ya Ushirika, wametoa jumla ya shilingi bilioni 10.2 pamoja na wataalam wa kusimamia uendeshaji wa taasisi muhimu za ushirika.

“Benki ya CRDB ilitoa shilingi bilioni 3.2 kwa Benki ya Wananchi Tandahimba (TACOBA) na shilingi bilioni 7 kwa Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL) pamoja na wataalamu wanaosaidia kwenye shughuli za uendeshaji kwa taasisi hizi zikiwa ni juhudi za kufufua ushirika nchini na kuziwezesha zijiendeshe kwa faida na tija zaidi,” amesema Wagana. 

Wagana amesisitiza kuwa “uwekezaji huu ndio unaochagiza kuanzishwa kwa Benki ya Taifa ya Ushirika. Bodi ya wakurugenzi, menejimenti na wafanyakazi wa Benki ya CRDB tunajivunia mafanikio haya ambayo kwa miaka ijayo, yatakuwa na mchango mkubwa kwenye kipato cha mwanaushirika mmojammoja na kuimarisha uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla.”

Vilevile, Wagana amesema Benki ya CRDB inawawezesha wakulima kupata pembejeo za kilimo hivyo kulima na kuongeza uhakika wa mavuno pamoja na kuwaunganisha na wanunuzi wa mazao yao kutoka ndani na nje ya nchi. 
“Hadi Juni, Benki ya CRDB imetoa mikopo yenye thamani ya  Shillingi trilioni 1.81 sawa na asilimia 43% ya mikopo yote itolewayo na mabenki kwenye sekta ya kilimo nchini. 

Kati ya mikopo hiyo tuliyoitoa,  shilingi bilioni 944.6 zimeelekezwa kwa wakulima wadogo ambao ni wanachama wa vyama vya ushirika (AMCOS) zipatazo 541 ili kuongeza tija kwenye uzalishaji kwa kununua pembejeo za kisasa, kujenga maghala, kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao, miradi ya ufugaji, na uwekezaji kwenye misitu, uvuvi na biashara,” amesema Wagana. 

Maonyesho ya Siku ya Ushirika Duniani yalifunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Juni 29 na kuhitimishwa Julai 5 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko.

Post a Comment

0 Comments