About Me

header ads

Mabadiliko ya Sheria ya Madini yawabeba Watanzania - Mavun

 

ARUSHA




MABADILIKO ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 yametoa fursa ya kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na kuhakikisha watanzania wananufaika na rasilimali madini.

Hayo yamesemwa leo Mei 22, 2024 na Waziri wa Madini. Mhe. Anthony Mavunde katika ufunguzi wa Jukwaa la Tatu la Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini linaloendelea kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano AICC jijini Arusha.
Waziri Mavunde amesema kuwa, katika mabadiliko hayo suala la Ushirikishwaji wa Watanzania limepewa kipaumbele ili kuhakikisha wawekezaji wote wanaojihusisha katika mnyororo wa uzalishaji na biashara ya Madini wanatoa kipaumbele kwa Watanzania.

“Marekebisho ya mwaka 2017 ya Sheria ya Madini, yalipelekea kutungwa kwa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za Mwaka 2018 ili kuweka usimamizi thabiti katika utekelezaji wa masuala ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini nchini,” amesema Mhe. Mavunde na kuongeza,
“Kulikuwa na malalamiko mengi, watanzania walikuwa ndugu watazamaji mpaka vyakula vilikuwa vinatoka nje, lakini baada ya mabadiliko ya sheria ya mwaka 2017 ushirikishwaji wa watanzania umekuwa mkubwa sana sambamba na watanzania kushika nafasi za juu za uongozi kwenye kampuni za madini,”amesema Mhe. Mavunde.

Amesema kuwa, katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Machi, 2024, Wizara kupitia Tume ya Madini ilipokea na kupitia jumla ya mipango 801 ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika shughuli za Madini sawa na ongezeko la asilimia 57 ikilinganishwa na mipango 510 iliyopokelewa katika kipindi kama hicho kwa Mwaka wa Fedha uliopita.

“Hii ni wazi kuwa mwamko wa Watanzania katika kushiriki fursa zilizopo kwenye Sekta ya Madini unakua kwa kasi,”amesema Mhe. Mavunde.

Amesema kuwa Wizara kupitia Tume ya Madini imeendelea kuhakikisha kuwa Watanzania wanapatiwa kipaumbele katika fursa za ajira zinazozalishwa katika migodi mikubwa na ya kati ya uchimbaji madini hapa nchini.

Ameendelea kusema kuwa hadi kufikia Machi, 2024 jumla ya ajira rasmi 19,358 zilizalishwa katika migodi hiyo ambapo ajira 18,853 sawa na asilimia 97 zilitolewa kwa Watanzania na ajira 505 sawa na asilimia 3 zilitolewa kwa wageni.

Pia amesema kuwa ajira kwa watanzania kwenye migodi zitaendelea kuongezeka ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Madini Sura 123 na Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za Mwaka 2018.

Aidha, amesema kuwa Wizara kupitia Tume ya Madini imeendelea kusimamia ununuzi wa bidhaa na huduma kwa kuhakikisha kipaumbele kinatolewa kwa watanzania kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura ya 123.

Amesema, usimamizi huo umekuwa na matokeo chanya kwa kuongeza idadi ya watanzania wanaotoa huduma na kuuza bidhaa kuanzia migodi ya uchimbaji mdogo, ya kati hadi ya uchimbaji mkubwa wa madini nchini.

“Katika Mwaka 2023 kampuni za kitanzania ziliuza bidhaa na huduma migodini zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.48 ambayo ni sawa na asilimia 90 ya mauzo yote yaliyofanyika migodini yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.65,”amesisitiza Mhe. Mavunde.

Amehitimisha kwa kusema kuwa, mauzo hayo yaliyofanywa na kampuni za kitanzania kwa mwaka 2023 yalikuwa ni zaidi ya mauzo yaliyofanywa mwaka 2022 ambayo yalikuwa na thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.08 sawa na asilimia 86 ya mauzo yote ya Dola za Marekani bilioni 1.26.












Post a Comment

0 Comments