About Me

header ads

WATUMISHI NGORONGORO WAENDESHA ZOEZI LA KUPANDA MITI

 

Na Mwandishi wetu, Karatu - Arusha

Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Victoria Shayo amewataka watumishi wa Mamlaka hiyo kuonesha mfano kwa kupanda miti katika maeneo yao ili kuunga mkono  juhudi za serikali katika kutunza mazingira.
Akiongoza menejimenti na watumishi  wa Mamlaka hiyo kwenye zoezi la Upandaji miti kaimu Kamishna huyo  ametoa wito huo katika tukio la upandaji miti lililofanyika kwenye jengo jipya la makao makuu linalojengwa wilayani Karatu.

Kaimu Kamishna Victoria Shayo amewapongeza watumishi walioshiriki kwenye zoezi la kupanda miti na kuwataka kuwa mabalozi wa utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya sasa na vizazi vya baadaye. 

Kwa upande wake Kaimu Meneja idara ya Usimamizi wa Wanyamapori na Utafiti, Afisa Uhifadhi Mkuu Lohi Zakaria, alisema kwamba lengo la kupanda miti ni kuunga mkono jitihada za Serikali za utunzaji wa mazingira na kutekeleza agizo la Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango alilolitoa siku ya kuwekwa kwa jiwe la Msingi la jengo hilo.  

Akitoa taarifa ya zoezi hilo Afisa Misitu wa mamlaka hiyo Naaman Naman amesema kwamba jumla ya miti 200 imepandwa na watumishi hao ambapo itasaidia kudhibiti mmmonyoko wa udongo katika eneo hilo.

Zoezi hili la upandaji miti ni mwendelezo wa maadhimisho ya siku ya Misitu duniani ambayo huwa inaadhimishwa tarehe 21 mwezi wa tatu na Kitaifa inaadhimishwa tarehe 01 mwezi wa nne kila Mwaka ambapo kwa mwaka huu kitaifa maadhimisho hayo yalifanyika Same, Mkoani Kilimanjaro na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ilishiriki na kugawa miche ya miti 3,100.





 

Post a Comment

0 Comments