About Me

header ads

TARANGIRE YAITA WAWEKEZAJI UTALII UKANDA WA KIMOTOROK

 

 

Na Seif Mangwangi, Manyara


Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), limeanza mchakato wa kufungua njia ya utalii ukanda wa kusini mwa hifadhi ya Taifa Tarangire baada ya kufanikiwa kumaliza mgogoro wa mpaka wa Kijiji Cha Kimotorok na hifadhi uliodumu kwa zaidi ya miaka kumi.

Kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Mkuu wa hifadhi ya Taifa Tarangire, Beatrice Kessy, hatua hiyo ya Shirika inatokana na kuanza kurejea kwa Wanyamapori katika ukanda wa kusini mwa hifadhi hiyo baada ya kumalizika kwa zoezi la kuondoa wananachi waliokuwa wakivamia eneo hilo kinyume Cha Sheria na kuweka mipaka ya kudumu.

Amesema Shirika lilishindwa kuwekeza utalii ukanda wa kusini mwa hifadhi hiyo kufuatia kuwepo kwa mgogoro wa mpaka kati yake na Kijiji Cha Kimotorok lakini ujio wa timu ya Mawaziri nane wa kisekta mwaka 2018, ambao waliagiza eneo hilo liwekwe mipaka ya kudumu na wananchi warejeshewe sehemu ya Ardhi umefanikiwa kutatua mgogoro huo.

" Tunashukuru sana ujio wa Mawaziri nane wa kisekta ambao waliagiza tuweke mipaka ya kudumu katika eneo hilo na tulifanikiwa kulima Mkuza wa zaidi ya kilometa za mraba 245 kati ya km251 , na pia tuliwarejeshea wananchi ekari 4392 ambazo zilikuwa sehemu ya hifadhi,"Anasema Beatrice Kessy.

Anasema hivi sasa wananchi wanaheshimu eneo la hifadhi kwa kutoingiza mifugo wala kufanya shughuli za kilimo kama ilivyokuwa hapo mwanzo jambo ambalo limesaidia kuongezeka kwa idadi kubwa ya wanyamapori katika ukanda huo ikiwemo makundi makubwa ya Tembo.

" Hivi Sasa tunakaribisha wawekezaji waje kuwekeza katika ukanda wetu wa kusini mwa hifadhi ya Taifa Tarangire, eneo hilo limeanza kuwa na wanyamapori wengi sana ambao ni kivutio kikubwa kwa watalii, sisi kama Shirika tumeanza mikakati ya kufungua njia upande huo ili kurahisisha shughuli za utalii,"Amesema.

Mkuu wa idara ya Himasheria katika hifadhi ya Taifa Tarangire, Mhifadhi Maria Kirombo Saidia ametoa wito kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi kulima zao la ufuta kwa kuwa wanyama wanaokula mazao kama tembo hawalidhuru.

" Wakati tunaondoa wananchi waliovamia eneo la hifadhi kulikuwa na mashamba ya wananchi ambayo tuliyaacha yaendelee mpaka watakapovuna, wale waliolima ufuta mazao yao yaliendelea pasipo kuathiriwa na wanyama tofauti na waliokuwa wamepanda mazao mengine, kwa hiyo tunashauri wananchi wanaoishi Karibu na hifadhi walime ufuta,"amesema Miriam.

Afisa Mhifadhi daraja la pili na Msimamizi wa mahusiano ya jamii hifadhi ya Taifa Tarangire, Fabian Nyakoro amesema baada ya kumalizika kwa zoezi la kuweka mpaka wa hifadhi na wananchi, hivi Sasa Shirika limeanza kutoa misaada ya huduma za kijamii kwenye vijiji vilivyokuwa na migogoro katika eneo hilo sanjari na kuweka mikakati ya pamoja ya ulinzi shirikishi.

Amesema kwa kipindi kifupi Tanapa imeweza kujenga nyumba mbili za walimu katika shule ya msingi Oltotoi, madarasa na ofisi ya Kijiji Cha Kimotorok sanjari na kusaidia Kijiji kutengeneza mpango bora wa matumizi ya Ardhi.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Mkuu wa hifadhi ya Taifa Tarangire, Beatrice Kessy akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na faida iliyopatikana baada ya kumalizika kwa mgogoro kati ya hifadhi na Kijiji Cha Kimotorok

Post a Comment

0 Comments