Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi , amewatembelea wananchi waliopatwa na maafa ya kuharibikiwa kwa nyumba na mali zao mara baada ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Nchini na kusababisha maporomoko ya matope kutoka kwenye mlima hali iliyopelekea uharibifu wa nyumba katika makazi ya wananchi wa mtaa wa Gomba kaskazini katika Kata ya Itezi.
Mara baada ya kufika katika kambi waiishio kwa muda katika shule ya msingi ya Tambukareli , Balozi Dkt. Nchimbi ametanguliza salamu za pole za Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan , na kuwapatia kiasi cha Tsh Milioni 10 wahanga hao ilikusudi kuendelea kuwawezesha katika nyakati hizi ngumu za mpito pesa ambazo zilikabidhiwa kwa mwanamama mmoja kati ya waliopatwa na maafa hayo pamoja na Diwani wa kata hiyo ya Itezi Ndugu. Sambweshi Tambala ambaye pia amepatwa na maafa hayo.
Akizungumza na Wananchi hao, Balozi Dkt. Nchimbi amesema lengo la kufika hapo ni kuwapa pole na kuwaomba kuendelea kumtanguliza na kumshukuru Mwenyezi Mungu bila kuacha kuomba usiku na mchana.
" Tumshukuru Mungu wote mpo salama, tujaribu kufikiria maporomoko haya yangetokea saa 8 usiku leo tungekuwa tunazungumza nini ? Tumtangulize Mungu sana "
" CCM inatoa shukrani kwa watu wote walioguswa na kuja kusaidia jambi hili, Shukrani pia kwa Serikali, Taasii mbalimbali na Mbunge wenu Dkt. Tulia Ackson "
" Niwaombe sana ndugu zangu, zingatieni tahadhari za serikali wakati uchunguzi unaendelea, wananchi tuwe na subira tusiharakie kurudi huko "
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Ndugu. Beno Malisa, amemueleza Katibu Mkuu kuwa maporomoko ya matope kutoka mlimani yalitokea siku ya jumapili tarehe 14 Aprili, 2024 na kusababisha uharibifu wa nyumba 21 na mali pekee bila kupelekea majeruhi wala vifo. Mafuriko hayo yamesababisha kaya zaidi ya 96 kukosa makazi hali iliyopelekea serikali kufanya juhudi za kuwapa makazi ya muda kwa kuweka kambi katika shule ya msingi ya Tambukareli.
DC Malisa ameendelea kusema kuwa wananchi hao wamepewa misaada ya huduma za kibanadamu kutoka serikali ya mkoa Mbeya na wadau mbalimbali.
Vilevile , DC Malisa amesema wananchi hao wamekuwa wakipatiwa huduma za afya na msaada wa kisaikolojia, Aidha shughuli zinazoendelea kwasasa ni kuweka sawa miundombinu ya umeme, maji na barabara.
0 Comments