About Me

header ads

WAJASIRIAMALI WAMSHUKURU RAIS SAMIA KUWAWEZESHA KUSHIRIKI MAONESHO YA JUAKALI BURUNDI

 

Na; Mwandishi Wetu – Bujumbura, BURUNDI

WAJASIRIAMALI kutoka maeneo mbalimbali nchini Tanzania wamemshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kushiriki maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu Nguvu Kazi au Jua Kali yanayofanyika Bujumbura, Burundi kuanzia tarehe 5 hadi 15 Desemba, 2023.

Wakizungumza Wajasiriamali hao kwa nyakati tofauti wamesema uratibu uliofanywa na Serikali kugharamia usafiri wao na mizigo, hali hiyo imewapa chachu ya kushiri kwa wingi zaidi. Pia, wamepongeza juhudi nahatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali chini ya uongozi Madhubuti wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kushiriki maonesho hayo.

“Sisi wajasiriamali tunafarijika sana kuona serikali yetu inatujali sana kwa kutupatia fursa hii muhimu ili tuweze kutangaza biashara zetu katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema Bi. Ester Ngalawa

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Ally Msaki amesema Serikali imeendelea kuwezesha Wajasiriamali Wadogo na wa Kati kutangaza biashara zao nje ya mipaka ya Tanzania.

Sambamba na hayo amehamasisha wananchi wa Burundi kutenmbelea mabanda ya wajasiriamali wa Tanzania ili kujionea bidhaa za ubunifu zinazozalishwa na wajasiriamali hao.

Naye Afisa Biashara Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Monica Miyigo amesema maonesho hayo yamevutia Wajasriamali Zaidi ya 1,500 kutoka nchi zote saba (7) wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Maonesho hayo yanaongozwa na kauli mbiu “Kuunganisha Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki kufanya biashara katika eneo la Jumuiya ya Afrika Mashariki,”. Yanalenga kutoa fursa kwa wajasiriamali kuonesha huduma na bidhaa mbalimbali wanazozalisha, kubadilisha uzoefu, ujuzi na taarifa na wajasiriamali wenzao katika Jumuiya sambamba na kukuza wigo wa masoko mapya.





Matukio katika picha Wajasiriamali wakiendelea na shughuli mbalimbali katika Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu Nguvu Kazi au Jua Kali yanayofanyika Viwanja vya Cercle Hyppique (Golf Course), Bujumbura, nchini Burundi.

Post a Comment

0 Comments