About Me

header ads

Benki ya CRDB yazindua Mikopo Maalum ya Hajj na Umrah isiyo na dhamana kusaidia Mahujaji kutekeleza ibada za Hija na Umrah

 

Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa Mikopo ya kuwawezesha mahujaji kwenda kwenye ibada za "Hajj na Umrah" ya Benki ya CRDB kupitia CRDB Al Barakah Banking, uliofanyika leo kwenye Makao Makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam leo. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Bonaventure Paul (wapili kushoto), Mjumbe wa Baraza la Ulamaa na Naibu Kadhi, Sheikh Ally Hamis Ngeruko (wakwanza kushoto), na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha CRDB Al Barakah Banking, Muhsini Said (kulia).
 
Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Bonaventure Paul (katikati) akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa Mikopo ya kuwawezesha mahujaji kwenda kwenye ibada za "Hajj na Umrah" ya Benki ya CRDB kupitia CRDB Al Barakah Banking, uliofanyika leo kwenye Makao Makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam. Kulia ni Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally pamoja naye ni Mjumbe wa Baraza la Ulamaa na Naibu Kadhi, Sheikh Ally Hamis Ngeruko.
 
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha CRDB Al Barakah Banking, Muhsini Said (kulia) akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa Mikopo ya kuwawezesha mahujaji kwenda kwenye ibada za "Hajj na Umrah" ya Benki ya CRDB kupitia CRDB Al Barakah Banking, uliofanyika leo.

========    ========    ========

Dar es Salaam, 10 Mei 2023 - Dar es Salaam, Tanzania – Katika jitihada zake za kupanua wigo wa kuwahudumia wateja Benki ya CRDB leo imezindua mikopo maalum ya Hija na Umrah, ambao unalenga katika kuwawezesha waislamu kufikia malengo yao ya kufanya kwa gharama nafuu.

Mikopo hiyo ya Hija na Umrah imekuja kama suluhisho kwa waumini wa dini ya kiislam ambao wanataka kufanya safari ya hija lakini wanakabiliwa na changamoto za kifedha. Kupitia mikopo hiyo, Benki ya CRDB inatoa suluhisho rahisi na nafuu, ambayo inawawezesha wateja kulipia gharama zao za usafiri na malazi.

Uzinduzi wa bidhaa hii mpya umekuja wakati mwafaka  ambapo Waislamu kutoka sehemu mbalimbali duniani wanajiandaa kutekeleza wajibu wao wa kuhiji. Mwaka huu, Tanzania ina nafasi ya kupata hadi mahujaji 3,000, lakini wengi wao hawana fedha za kutosha kufadhili safari yao.

"Tunafurahi kuja na ubunifu huu wa mikopo Hajj na Umrah kama nyongeza kwenye bidhaa zetu za CRDB Al Barakah Banking. Mikopo hii inathibitisha dhamira yetu ya kutoa ufadhili nafuu za ufadhili kwa wateja wetu wote, hasa wale wanaotaka kutekeleza ibada ya Hijja na Umrah," alisema Bonaventura Paul.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha CRDB Al Barakah Banking, Muhsin Said alisema mikopo hiyo ya Hajj na Umrah inatolewa kwa masharti nafuu kwani haihitaji dhamana yoyote, hivyo kutoa fursa kwa Waislamu wote nchini kunufaika.

“Mikopo hii inatolewa hadi shilingi milioni 30. Kwa wateja wafanyakazi Benki inafanya uwezeshaji wa hadi asilimia 80 ya gharama zote za safari na kwa wafanyabiashara na wajasiriamali Benki inatoa uwezeshaji wa hadi asilimia 50 ya gharama zote za safari,” alisema Muhsin.

Katika hafla hiyo ya uzinduzi, Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuanzisha mikopo hiyo ya ufadhili wa Hija na Umrah, huku akiwahamasisha Waislam kote nchini kutumia fursa hiyo kutimiza ibada za Hija na Umrah.

"Huu ni mpango mzuri sana kutoka Benki ya CRDB, na nawapongeza kwa kuja na ubunifu huu. Ninahimiza Waislamu wote wa Tanzania kutumia fursa hii," alisema Sheikh Abubakar Zubeir huku akiiomba Benki ya CRDB pia kuziwezesha taasisi za mahujaji nchini.

Uzinduzi wa mikopo ya ufadhili wa ibada za Hija na Umrah unasisitiza zaidi dhamira ya Benki ya CRDB katika kutoa masuluhisho ya kifedha ya kibunifu na jumuishi kwa wateja wote. Kupata huduma za mikopo hiyo, wateja wanatembelea tawi lolote la Benki ya CRDB.

Benki ya CRDB ilizindua huduma zake za “CRDB Bank Al Barakah,” mwaka 2021 ambapo hadi sasa tayari imevutia wateja zaidi ya wateja 30,000 ambao wamenufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa zikiwemo akaunti na mikopo.

Ripoti ya Benki hiyo inaonyesha kuwa Benki ya CRDB kupitia Al Barakah Banking imetoa zaidi ya Shilingi bilioni 73 kwa wateja tangu kuanzishwa kwake, jambo linaloonyesha ongezeko la mahitaji ya huduma za kibenki zinazofuata msingi ya kiislamu nchini Tanzania.

Post a Comment

0 Comments