ROBERTINHO AMUWEZA NABI
Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
SIMBA SC imefanikiwa kuondoka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya watani wao wa jadi, Young Africans SC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (NBC Premier League) uliopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo ambao uliokuwa wa ushindani muda wote wa dakika 90’, mabao ya Simba SC yalifungwa dakika za mapema kupitia kwa Mlinzi wa timu hiyo, Henock Inonga Baka kwenye dakika ya 2’ huku bao la pili likifungwa na Mshambuliaji Kibu Dennis kwenye dakika ya 31’ mchezo.
Mchezo huo ulienda mapumziko kwa Simba SC kuwa mbele na uongozi wa mabao 2-0 dhidi ya Young Africans SC kwenye dimba hilo la Benjamin Mkapa. Hata hivyo, Wekundu wa Msimbazi walikosa mabao mengine ya wazi katika kipindi hicho cha kwanza ambayo yalikoswa na Mshambuliaji Jean Baleke.
Licha ya kipigo hicho, Young Africans SC walicheza vizuri na walitawala mchezo huo hususani kwenye kipindi cha pili cha mchezo, vile vile ubora huo ulichagizwa na mabadiliko yaliyofanyika kwa kuingia kwa Wachezaji, Stephane Aziz Ki, Mudathir Yahya, Tuisila Kisinda na Bernard Morrison ambao wote walileta mabadiliko kwenye safu ya ushambuliaji ya Yanga SC.
Hata hivyo, Simba SC walicheza kww tafadhari kubwa katika vipindi vyote vya mchezo huo, wakiwazuia Wananchi wakati wote licha ya Wananchi kufanya mabadiliko katika kipindi cha pili ili kuongeza nguvu katika nafasi ya Kiungo na safu ya ushambuliaji.
Kwa ushindi huo, Simba SC wameendelea kuwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na alama 63 wakiwa na michezo 26 sawa na Young Africans wenye michezo kama hiyo wakiwa nafasi ya kwanza na alama zao 68.
Mara ya mwisho Simba SC kupata ushindi mbele ya Young Africans SC kwenye Ligi Kuu Soka Tanzania Bara ilikuwa Februari 16, 2019 ambapo walipata ushindi wa bao 1-0 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, bao pekee la Simba SC lilifungwa na Mshambuliaji wa wakati huo, Meddie Kagere.
Simba SC waliwahi kupata ushindi kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) kwenye Nusu Fainali ya Michuano hiyo, Julai 12, 2020 walipata ushindi wa mabao 4-1 na walipata ushindi wa bao 1-0 kwenye Fainali ya Michuano hiyo kwenye uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, Julai 25, 2021.Mlinzi wa Simba SC, Henock Inonga Baka akishangilia bao la kwanza la kichwa alilofunga kwenye dakika ya 2’ ya mchezo dhidi ya Young Africans SC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, uliopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mshambuliaji wa Simba SC, Kibu Dennis akishangilia bao la pili alilofunga kwenye dakika ya 31’ kwenye mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Simba SC waliondoka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya mtani wao, Yanga SC
0 Comments