About Me

header ads

GGML YAUNGA MKONO JITIHADA KUPANDA MITI HALMASHAURI YA MBOGWE

Na Mwandishi Wetu

WAKATI Tanzania ikiadhimisha Siku ya Upandaji Miti Kitaifa ambayo ni Aprili 1, 2023, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imeahidi kudumisha dhamira yake ya kulinda na kuhifadhi uoto wa asili katika eneo lake lenye leseni ya uchimbaji madini.


Itakumbukwa kuwa, Hifadhi ya Msitu wa Geita ni sehemu ya eneo hilo lenye leseni maalum ya uchimbaji madini ya GGML.

Siku ya kitaifa pia hutumika kukumbusha jamii na wadau umuhimu wa miti na uhifadhi wa misitu.Kaulimbiu ya mwaka huu katika Siku ya Kitaifa ya Kupanda Miti ni “Tanzania ya Kijani, Hakuna Miti, Hakuna Uhai.”

Akizungumza katika maadhimisho ya siku hiyo yaliyofanyika ki-mkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Ofisa Mwandamizi wa Uhusiano wa Umma wa GGML, Musa Shunashu amesema uendelevu wa kimkakati ni miongoni mwa maadili ya Kampuni iliyozinduliwa hivi karibuni ambapo kuheshimu mazingira ni sehemu muhimu.

"Kimaadili, tunalazimika kufanya biashara yetu kwa kuzingatia hali ya mazingira na jamii ambayo ni mambo muhimu katika bioanuwai. Tumekuwa tukiendesha programu kadhaa za upandaji miti ili kurejesha mazingira tunamofanyia shughuli zetu za uchimbaji madini.

“Katika msimu wa mvua wa 2022/23, GGML imepanda jumla ya miti 168,500 kama sehemu ya mpango wa kurejesha uoto. Ikumbukwe kuwa zaidi ya asilimia 76 ya Leseni yetu ya Uchimbaji Maalumu ipo ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Geita, hivyo kupanda miti kwa ajili ya kurejesha asili ni jambo la muhimu,” amesema.

Ameongeza katika maadhimisho ya mwaka huu, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited iliamua kusambaza miche 14,000 ya miti kwa wafanyakazi wake na wakandarasi ili kusaidia mipango ya serikali ya kupanda miti mingi.

"Mwaka huu tunatumia msimu wa mvua kupanda miti na tumesambaza miche kwa wafanyakazi wetu na wakandarasi," amesema Shunashu.

Akiongoza hafla ya upandaji miti eneo la Kashelo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, aliipongeza GGML, Hifadhi ya Misitu Tanzania na wadau wengine kwa kuwa mabalozi wazuri wa kuheshimu mazingira.

"Tulizindua mpango maalum wa kupanda miti kama ilivyoagizwa na Rais Samia Suluh Hassan mwaka jana kwamba kila halmashauri inapaswa kupanda miti isiyopungua Milioni 1.5. Tunafurahi kwamba kwa kushirikiana na washirika wetu wakuu kama GGML, mkoa wetu umefikia 33% ya lengo," amesema.

Mwaka 2022 pekee, GGML ilipanda miti zaidi ya 3,500 na kusambaza aina 7,000 za miche ya matunda katika mji wa Geita. Wakati wa Kongamano la Nne la Kimataifa la Uwekezaji wa Madini Februari 2022, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliitambua GGML kama Mshindi wa Nafasi ya Kwanza kati ya Wamiliki wa Leseni Maalum za Uchimbaji kwa uzingatiaji wa Sheria zinazohusu masuala ya mazingira na usalama.
Ofisa Mwandamizi wa Uhusiano wa Umma wa GGML, Musa Shunashu akipanda mti katika eneo la Mbogwe mkoani Geita huku akishuhudiwa na Mkuu wa mkoa huo Martin Shigela ikiwa ni maadhimisho ya siku ya upandaji miti kitaifa.
Mkuu mkoa wa Geita Martin Shigela akipanda mti katika eneo la Mbogwe mkoani humo katika maadhimisho ya siku ya upandaji miti kitaifa.
Ofisa Mwandamizi wa Uhusiano wa Umma wa GGML, Musa Shunashu akipanda mti katika eneo la Mbogwe mkoani Geita huku akishuhudiwa na baadhi ya maofisa maliasili ikiwa ni maadhimisho ya siku ya upandaji miti kitaifa.

Post a Comment

0 Comments