NCHI ya Tanzania wakati huo ikiwa chini ya uongozi wa Rais wa Awamu ya
Kwanza Hayati Mwl.Julius Nyerere ilishiriki kikamilifu kwenye harakati za
ukombozi kusini mwa Afrika.
Nchi ya Msumbiji ni miongoni mwa nchi ambazo hazitaisahau Tanzania
ilivyotoa mchango wake hadi kusababisha nchi hiyo kupata uhuru wake
toka kwa wareno mwaka 1975.
Alfonso Kaidavid ni Mhifadhi kwenye makumbusho ya Taifa ya Msumbiji
yaliyopo Matchedje Jimbo la Niassa, anasema serikali ya Msumbiji
imeamua kuanzisha makumbusho katika eneo hilo kutokana na kufanyika
mkutano wa pili mwaka 1968 uliosababisha nchi hiyo kupata uhuru wake.
Anasema mkutano wa kwanza wa harakati za kuikomboa Msumbiji
ulifanyika jijini Dar es salaam nchini Tanzania mwaka 1962 ukiongozwa na
Rais Julius Nyerere wa Tanzania na viongozi waandamizi wa FRELIMO
nchini Msumbiji ambao ni Edwardo Mondlane na Samora Machel.
Mhifadhi Kaidavid anasema Mkutano wa pili ulifanyika kwa siku tano katika
eneo la Matchedje kuanzia Julai 20 hadi 25 mwaka 1968 na kwamba
mkutano huo ulioongozwa viongozi waandamizi wakiwemo Rais Julius
Nyerere wa Tanzania,Edwardo Mondlane na Samora Machel wa Msumbiji.
“Makumbusho haya tumeanzisha ili wanamsumbiji,watanzania na wageni
wengine kutoka nchi mbalimbali waweze kujua ni namna gani nchi ya
Msumbiji ilipambana katika kuikomboa nchi toka kwa wakoloni wareno
ambao walitutawala kwa miaka mingi’’,anasisitiza Kaidavidi.
Anamtaja kiongozi wa FRELIMO hayati Edward Mondlane kwa kushirikiana
na Samora Machel walipata mafunzo mbalimbali nje ya nchi ya Msumbiji
namna ya kumfukuza mkoloni ili kuiacha Msumbiji huru.
Mhifadhi huyo anasema kabla ya kuamua kumwaga damu viongozi hao
walijaribu kuzungumza na wareno ili wakubali kwa hiyari kutoa uhuru wa
Msumbiji,hata hivyo ilishindikana ndipo waliamua kutumia njia ya bunduki.
Historia inaonesha kuwa wareno walifika nchini msumbiji mwaka 1498 na
kwamba safari yao ilikuwa ni kwenda nchini India,hata hivyo waliamua
kubaki Msumbiji,baada ya kubaini nchi hiyo ina utajiri mkubwa wa madini
na meno ya tembo.
Akizungumzia vivutio vya utalii vilivyopo eneo hilo la kihistoria la
Matchedje,Kaidavid anasema kwenye eneo hilo yamebakia masalia ya
vibanda mbalimbali ambavyo viongozi wa kitaifa waliishi kwa siku tano
kufanya mkutano wa pili mwaka 1968 uliozaa uhuru wa Msumbiji.
Moja ya vivutio kwenye eneo hilo ni uwepo wa gogo ambalo mwaka 1968
walikalia Rais Julius Nyerere wa Tanzania,Rais Edward Mondlane wa
Msumbiji na Mkuu wa Majeshi alikuwa Samora Machel ambao walikaa
kwenye gogo hilo kwa siku tano wakijadili namna ya kuikomboa nchi ya
Msumbiji toka kwa wareno.
“Viongozi hao mwaka 1968 walijadili wakiwa wamekaa kwenye gogo hili
ambalo hadi leo bado lipo likiwa vile vile bila kuoza,tumelihifadhi kama
kumbukumbu muhimu kwenye harakati za ukombozi wa nchi ya
Msumbiji’’,anasisitiza Mhifadhi huyo.
Maeneo mengine ambayo ni kivutio kwenye eneo hilo ni uwepo wa kibanda
ambacho alilala kwa siku tano Rais wa Msumbiji Edwardo Mondlane
mwaka 1968,pia kuna kibanda ambacho alilala Mkuu wa Majeshi Samora
Machel kwa siku tano na kibanda ambacho walilala waandishi wa habari
kwa siku tano.
Ukiachia harakati zilizoendelea nchini Msumbiji, eneo la Masonya lililopo
katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma nchini Tanzania
lina utajiri wa utalii wa malikale na utambulisho wa Taifa,ingawa bado
halifahamiki na wengi.
Eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 100 lina vivutio adimu vya utalii wa
malikale ikiwemo nyumba yenye namba A 10 ambayo walikuwa wanafikia
na kuishi Marais Hayati Julius Nyerere wa Tanzania na Hayati Samaro
Machel wa Msumbiji kuanzia 1966 wakati wa harakati za ukombozi
Kusini mwa Afrika.
Mhifadhi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Bartazar Nyamusya
anasema viongozi hao pia wakiwa katika nyumba hiyo,walitumia jengo
dogo maalum lililopo jirani ya nyumba hiyo kama chumba cha
mawasiliano yote na nchi zilizokuwa katika harakati za ukombozi kusini
mwa Afrika.
Kutoka nyumba ya viongozi hao hadi jengo dogo la mawasiliano,lilijengwa
handaki la chini kwa chini ambalo lipo hadi sasa lililokuwa linatumiwa na
viongozi hao wa Tanzania na Msumbiji.
Historia inaonesha kuwa Rais wa sasa wa Msumbiji Pilipe Nyusi amesoma
shule ya msingi FRELIMO iliyokuwepo katika eneo la Masonya ambaye
alifika hapo mwaka 1970 akiwa na umri wa miaka nane.
Hata hivyo serikali hivi sasa inalitumia eneo la malikale la Masonya kwa
shughuli za kielimu ambapo katika eneo hili imejengwa shule ya sekondari
ya wasichana Masonya.
Kabla ya mwaka 1966,eneo la malikale la Masonya lilikuwa ni msitu
ambapo katika mwaka huo ndipo serikali iliwapokea watu kutoka nchini
Msumbiji na kuwakabidhi eneo hilo katika kipindi chote cha kupigania
uhuru nchini Msumbiji.
Nurdin Seleman ni Mwenyekiti wa kijiji cha Masonya anasema kijiji hicho
ilikuwa ni kambi ya wapigania uhuru wa nchi ya Msumbiji na kwamba eneo
hilo lina malikale mbalimbali zilizokuwa zinatumiwa na wananchi wa
Msumbiji.
Anasema eneo hilo linatembelewa mara kwa mara na wananchi wa
Msumbiji akiwemo Balozi wao ambapo serikali ya kijiji hicho inaendelea
kuzitunza malikale hizo ambazo ni muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo
kwa maendeleo ya nchi zote mbili.
Katika kipindi cha miaka kumi kuanzia 1966,wanawake toka nchini
Msumbiji wamekuwa wanaishi katika eneo la Masonya,Umoja wa
Wanawake wa Msumbiji unaojulikana kwa OMM ulianzia Masonya mwaka
1973.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro anazitaja rasilimali adimu
zilizopo katika eneo la malikale la Masonya kuwa ni majengo 13 ya
FRELIMO na masalia ya kale ya nyumba za viongozi wa kitaifa ambao ni
Hayati Julius Nyerere na Samora Machel.
0 Comments