About Me

header ads

NCHI KUMI ZA AFRIKA ZANUFAIKA NA UTAFITI WA TANZANIA

Kiongozi wa Sekretarieti ya Azimio la Nairobi Bw. Dixon Waruinge ambaye ndiye Msimamizi wa Utekelezaji wa Mradi wa Mfano wa Tathimini ya Maji kwa Mazingira (EFLOWS) amesema mradi huo umetekelezwa vizuri zaidi ya vile walivyotarajia na matokeo yake yameshaanza kunufaisha baadhi ya nchi za Afrika.

Kiongozi huyo ameyasema hayo mkoani Njombe kwenye wilaya ya Wanging`ombe mara baada ya yeye na timu ya maafisa wengine wa sekretarieti hiyo ya Azimio la Nairobi kumaliza kazi ya kukagua na kuona kazi mbalimbali zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa naMradi huo unaotekelezwa na Watafiti wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa kushirikiana na Baraza la Hifadhi ya Mazingira NEMC kwenye Wilaya za Mbarali na Wangingombe mkoani Njombe na Mbeya.

“La muhimu au kubwa zaidi ni kusema kuwa Tanzania mmefanikisha kuzidi kiasi ambacho tulitarajia, utafiti umefanyika vizuri sana na tayari kuna nchi zimenufaika na masomo (leasons) kutoka Tanzania maana Prof. Japhet Kashaigili amesafiri kwenda Madagasca kuwapa masomo yaliyopatikana Tanzania, na sisi hapa tumezishuhudia na baada ya hapa nchi nyingine nyingi zitajifunza kutokana na mambo waliyofanya Tanzania”, alifafanua Bw. Waruinge.

Kiongozi huyo wa Azimio la Nairobi amesema umuhimu wa azimio hilo ambalo linaundwa na nchi 10 za Afrika Mashariki na Visiwa vya Madagascar, Seychelles na Comoros, Mauritius na Reunion ambayo ipo Ufaransa wakutane kama nchi wayaangazie masuala yote ya mazingira ya maji ya Bahari na wanapoangalia hayo lazima wazingatie na kutazama maji ya mito kwa kuwa maji yake pia yanaingia baharini.

Bw. Wariunge amesema kutokana na hilo wakaona ni vyema kuangalia ni kwa namna gani mito inahifadhiwa kwa ajili ya Mikoko na Samaki na baada ya kufikia hatua hiyo wakajiuliza suala la mito inayopita nchi moja na nyingine na mito ya ndani ya nchi moja kujua changamoto zake na namna inavyotunzwa.

“Kwa hiyo tukakubaliana tuwe na mradi ambao utaangazia masuala hayo kwa kuwa matatizo yanayogusa mito ya nchi moja yanalingana na ya nchi nyingine ndipo mradi huu ukaanzishwa na tukaona hatuwezi kuanzisha mradi kama huu nchi zote 10 ndipo Tanzania ikachaguliwa kutekeleza mradi huu wa mfano kupitia mto Rufiji na Mbarali kama chanzo cha utafiti na maarifa ya yale yatapatikana kama mafunzo Tanzania yasaidie kusambazwa kwenye serikali za nchi zingine zilizobaki Afrika”, alieleza Kiongozi huyo wa Sekretarieti ya Azimio la Nairobi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Makamu wa Rais upande wa Bionuai Bw. Thomas Bwana amesema kwenye eneo la mazingira kuna eneo kubwa wanaliangalia ambalo ni Vyanzo vya maji eneo ambalo maji yake yanakwenda kwenye mito na mwisho wake ni baharini hivyo lazima maeneo hayo yapewe kipaumbele.

“Eneo hili hapa tuliposimama ni chanzo kikubwa tu cha maji ambacho kilikuwa kimeharibiwa na shughuli mbalimbali za binadamu lakini kupitia kazi kubwa ya kutoa elimu kupitia mradi huu na wataalamu wengine unaweza kuona sasa limepandwa miti rafiki wa maji na linatunzwa hata zile shughuli za kibinadamu hazifanyiki tena mahali hapa na maji yanaendelea kutiririka na hii inatufundisha kuwa kumbe inawezekana wananchi kutunza vyanzo hivi vya maji kwa faida yao na taifa kwa ujumla”, alisema Bw. Thomas.

Ameongeza kuwa Mradi huu wa Utafiti wa EFLOWS unasaidia jamii na Tanzania kujihakikishia upatikanaji wa maji na utiririkaji salama kwa ajili ya matumizi ya kilimo kupitia umwagiliaji, Uzalishaji wa umeme kwenye maeneo mengine, Maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani katika maeneo yaliyo eneo la chini la mto na hilo ndio lengo kubwa kwa Ofisi ya Makamu wa Rais upande Mazingira.

Mkurugenzi huyo Msaidizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais upande wa Bionuai amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na watafiti wa SUA na NEMC katika kutekeleza mradi huo mzuri wa mfano na kuahidi kuendelea kushirikiana nao ili matokeo mazuri ya mradi huo yaweze kutumiwa pia kwenye maeneo mengine ya Tanzania yenye vyanzo vya maji na mito.

Kwa upande wake Mtafiti Mkuu wa Mradi huo kutoka SUA Prof. Japhet Kashaigili amesema chimbuko la mradi huo linaungana na utekelezaji wa Sheria ya Maji na Mazingira ambayo katika kugawana maji kuna vipaumbele vitatu ambavyo ni maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu, maji kwa ajili ya Mazingira na maji kwa ajili ya shughuli zingine.

“Ukiangalia mgawanyo huo wa maji ni rahisi kujua maji kwa ajili ya binadamu umetumia kiasi gani kwa siku lakini maji kwa ajili ya matumizi mengine kama vile kilimo pia ni rahisi kujua lakini maji kwaajili ya mzingira kutunza bionuai kwaajili ya sasa na baadae ni kama ilikuwa haijulikani au Sayansi yake haikuwepo lakini sasa utaalamu huu tunao na tumefanya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na duniani sasa nchi mbalimbali zinaweza kufanya tathmini hii ya maji kwa mazingira”, alifafanua Prof. Kashaigili.

Amesema kupitia utaalamu huo sasa wameweza kufanya tathimini hiyo kwenye mto Mbarali kuanzia juu kwenye vyanzo vya mto kufika katikati ambako jamii inatumia maji kwa kazi mbalimbali za kilimo, kuingia kwenye ardhi oevu, kuingia mto Rufiji hadi kwenye hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kwenda kwenye mabwawa ya uzalishaji umeme ya Kidatu na Mwl.Julius Nyerere na mwisho kuingia baharini.

Mtafiti huyo Mkuu amesema Mradi huo ni mfano kwa kuwa unamaanisha athari zitokanazo na shughuli za kibinadamu kwenye mtiririko wa maji kwenye mito na namna ya kupunguza athari hizo na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambao wana mahusiano ya moja kwa moja na maji hayo ya mto ikiwemo Jumuiya za watumia maji, Mamlaka ya Bonde la Mto Rufiji, TANAPA, TANESCO na wengine ikiwemo wakulima.

Mradi huo wa mfano wa utafiti wa “Usimamizi Endelevu wa Madakio ya Maji kwa kuimarisha Tathimini ya Mtiririko wa Maji ya Mazingira na Utekelezaji wa Mpango Mkakati kwa ajili ya Mazingira wenye Lengo la Kulinda Ukanda wa Magharibi wa Bahari ya Hindi kutokana na Athari za Shughuli za Kibinadamu, Tanzania” kwa ufadhiliwa na Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa kupitia ufadhili wa Program ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa, UNEP na kutekelezwa kupitia Sekretarieti ya Azimio la Nairobi.








Post a Comment

0 Comments