Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip
Mpango ameitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha ujenzi wa
barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu yenye urefu wa kilometa 260.6
unakamilika kwa wakati na ufanisi uliokusudiiwa.
Amesema hayo Wilayani Kasulu alipokutana na Wajumbe wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) na viongozi wa
Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na kusisitiza kuwa kukamilika kwa barabara
hiyo kwa kiwango cha lami ndio utakuwa ukombozi wa uchumi wa mkoa
wa Kigoma na kanda ya magharibi kwa ujumla.
“Wananchi wengi wa Kasulu, Kibondo na Kakonko wanafanya biashara
nyingi Kahama, Shinyanga na Mwanza hivyo kukamilika kwa barabara hii
kutakuza uchumi wa wakazi wengi wa mkoa wa Kigoma”, amesema Dkt.
Mpango.
Amesisitiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara
nchini (TANROADS), kuongeza kasi ili kukidhi matarajio ya Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan ya kuufungua Mkoa wa Kigoma katika Nyanja zote
za usafiri.
Naye Mwenyekiti wa PIC Mhe. Jerry Silaa amemweleza Makamu wa Rais
kuwa Kamati yake imekagua uwekezaji wa Serikali mkoani Kigoma na
imeridhika kwa kazi nzuri zinazofanywa katika usafiri wa reli, bandari,
barabara na anga na kumhakikishia Makamu wa Rais kuwa kamati hiyo
itakagua miradi hiyo mara kwa mara ili kuhakikisha uwekezaji unaofanywa
unakuwa na tija kwa wananchi.
“TANROADS hakikisheni ujenzi wa barabara licha ya kutoa fursa kwa
wananchi bali uwezeshe wakandarasi wetu kupata ujuzi na hivyo kumudu
kujenga na kusimamia miradi mikubwa siku za usoni”, amesesitiza Mhe.
Silaa.
Aidha, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya
ujenzi), Bw, Ludovick Nduhiye amesema Wizara imejipanga kuhakikisha
mkoa wa Kigoma unafikika kwa urahisi kupitia barabara zake zote, reli,
bandari na anga ili kuuunganisha na masoko ya nchi za Congo, na Burundi
kwa urahisi na hivyo kukuza shughuli za kilimo, biashara na uwekezaji.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Rogatus Mativila amesema barabara
ya Kabingo-Kasulu-Manyovu yenye urefu wa kilometa 260.6 ni sehemu ya
barabara kuu ya Nyakanazi-Kibondo-Kasulu-Manyovu inayounganisha
mkoa wa Kigoma na mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga na Mwanza na
pia inaunganisha Tanzania na Burundi kupitia mpaka wa Manyovu.
barabara ya kikanda yenye lengo la kuufungua ukanda wa magharibi na
kuiunganisha Tanzania na Burundi.
Eng. Mativila amesema katika kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo ya
kikanda unakwenda kwa haraka mradi umegawanywa katika sehemu nne
ambapo zaidi ya shilingi bilioni 325.6 zinatarajiwa kutumika katika kuwalipa
wakandarasi wanne wanaojenga barabara hiyo wakati takriban shilingi
bilioni 15.37 zikitengwa kuwalipa wasimamizi wake.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), iko
mkoani Kigoma kukagua utekelezaji wa miradi ya Serikali ambapo pamoja
na mambo mengine imekagua, imeelekeza na kuelezea kuridhishwa na
kasi ya ujenzi wa barabara hiyo ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lamiunatarajiwa kukamilika baadae mwaka huu.
Muonekano wa barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu yenye urefu wakilometa 260.6 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea
mkoani Kigoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akisisitiza jambo kwa Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Bw, Ludovick Nduhiye na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila
alipokagua barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu yenye urefu wa kilometa 260.6 Mkoani Kigoma.
0 Comments