About Me

header ads

MCHIMBAJI MADINI WA SINGIDA AMLILIA RAIS SAMIA AMSAIDIE KUPATA HAKI YAKE

 

Mchimbaji mdogo wa madini, Richard Lyamuya, mkazi wa Manispaa ya Singida, akizungumza na waandishi wa habari leo (Machi 21,2023) kuhusu madai ya Ofisi ya Madini Mkoa wa Singida kukataa kumpatia leseni ya uchimbaji wa madini.                                                                                        

Na Dotto Mwaibale, Singida

MCHIMBAJI mdogo wa madini, Richard Lyamuya, mkazi wa Manispaa ya Singida , amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati apate haki yake baada ya Ofisi ya Madini Mkoa wa Singida kukataa kumpatia leseni wakati amefuata taratibu zote kwa  kulipia ada  tatu zilizoainishwa kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari leo (Machi 21,2023) amesema alipeleka maombi ya kupatiwa leseni ya uchimbaji dhahabu katika kijiji Cha Matongo wilayani Ikungi ambapo ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Singida ilimwelekeza alipie ada ya maombi,ada ya maandalizi na ada ya pango na vyote alilipia kama kawaida na kupewa stakabadhi.

Lyamuya alisema katika hali ya kushangaza baada ya leseni kutoka ili akabidhiwa Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Singida, Chone Malembo, amekataa kusaini leseni iweze kutoka kwa madai eneo aliloomba lina mgogoro jambo ambapo limezua maswali yasiyo na majibu kwasababu kama ofisi hiyo ilijua eneo hilo lina mgogoro ni kwanini ilimruhusu kulipia ada hizo.

Alisema amefuatilia suala hilo kwa kuandika barua katika ofisi ya Madini Mkoa wa Singida,Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi na kwa Mkuu wa Mkoa lakini bahati mbaya hajapata msaada wowote.

'Katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi nimefika zaidi ya mara saba bahati mbaya sikufanikiwa kuonana na Mkuu wa Wilaya badala yake nilionana na Afisa Tawala ambaye alinisikiza na akanipa majibu kuwa ameongea na Afisa Madini wa  Mkoa wa Singida  akasema leseni ninayoilalamikia hataweza kunipa bali niendelee na leseni nyingine nilizonazo," alisema Lyamuya.

Aliongeza jambo la kushangaza wakati tayari ameshafanyiwa mchakato na kusubiri kupata leseni baadhi ya maofisa katika ofisi ya Madini Mkoa wa Singida waliweka ombi namba PML145961/CZ Septemba 3 mwaka jana kwenye mtandao katika eneo hilo hilo ambalo yeye ameomba leseni lakini baadaye ombili hilo liliondolewa..

Lyamuya alisema baada ya kufika katika ofisi zote za serikali bila mafanikio Machi 13, mwaka huu mwanasheria wake wa kampuni ya Kim & Co Advocates aliiandikia barua ofisi ya Madini Mkazi Mkoa wa Singida kutaka mteja wao apewe leseni yake kwa kuwa amefuata taratibu zote.

"Unachokifanya sio matakwa ya sheria bali ni utashi wako kama mtu binafsi,hakuna mgogoro wa kiuchimbaji katika leseni hii na hata mgogoro ungekuwepo basi kifungu cha 102 cha sheria ya Madini namba 14 ya 2010 kingetumika na kwa niaba ya Kamishina wa Madini ungeendesha nafasi hii ya kimahakama na kutoa maamuzi ya mgogoro lakini tunachokiona unashughulika na upande mmoja wa mteja wetu," imeeleza sehemu ya barua hiyo ambayo ameandikiwa Afisa Madini Mkoa wa Singida.

Mwanasheria wa mchimbaji huyo Raymond Kim, amendelea kueleza katika barua yake hiyo  kwa kutoa angalizo kwamba mteja wao atawajibika kuchukua hatua za kisheria kama ofisi ya Madini Mkoa wa Singida itaendelea kukataa kutoa leseni namba PML 0734SGD ambayo leseni hiyo ilitokana na ombi namba PML 133372/CZ.

"Hatua itakayofuata ni kufungua kesi mahakamani dhidi yako wewe binafsi na kuwajibika kulipia fidia zote za kisheria ikiwa ni pamoja na hasara na gharama za kesi," imeeleza barua hiyo kwenda kwa Afisa Madini Mkoa wa Singida.

Kufuatia hali hiyo,amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati suala hilo kwakuwa amefuatilia katika ofisi nyingi za serikali na hajapata msaada.

Kaimu Afisa Madini Mkoa wa Singida, Chone Malembo, alipoulizwa alikiri kuufahamu mgogoro huo na kuwa ulianza baada ya watu wawili kujitokesa kwamba eneo hilo aliloomba leseni Lyamuya (mchimbaji) ni shamba lao.

Alisema walibaini eneo aliloomba  Lyamuya lina mgogoro wakati tayari ameshafanya mchakato wa malipo na alipoulizwa na waandishi kama je fedha hizo atarudishiwa mchimbaji huyo alijibu hilo ni suala jingine bila ya kufafanua zaidi.

Malembo alisema ofisi yake itaendelea kufanya mchakato wa kusuluhisha kati ya wenye shamba ambao nao wanataka wafanye uchimbaji kwenye eneo hilo kama wataona inafaa wafanye ubia wa uchimbaji.

Mkaguzi Mkuu wa mgodi huo, Japhet Madusa akizungumzia changamoto iliyojitokeza katika eneo hilo. alisema katika migodi mbalimbali ambayo amewahi kufanya kazi mmiliki wa shamba amekuwa akipewa asilimia 10 hadi 20  na mwekezaji mwenye leseni  lakini imekuwa tofauti katika mgodi huo ambapo mwenye shamba anataka apewe mgao sawa na mwekezaji jambo ambalo linaleta changamoto.

Mkaguzi Mkuu wa mgodi huo, Japhet Madusa akizungumzia changamoto iliyojitokeza katika eneo hilo.

Msimamizi wa ugawaji mawe katika mgodi huo, Rajabu Lue,akizungumzia mgogolo huo.
Mmoja wa wamiliki wa shamba hilo, Israel Njiku akizungumzia mgogoro huo alisema kuwa walifanya utaratibu wote wa uchimbaji ikiwa ni pamoja na kulipia malipo yaliyokuwa yakihitajika.
Muonekano wa maeneo kadhaa ya mgodi huo.
Taswira ya mgodi huo.
Muonekano wa mgodi huo.
 

Post a Comment

0 Comments