Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wake Mhe. Japhet Hasunga imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mabweni ya Chuo cha VETA cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC).
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua mradi huo leo tarehe 19 Machi, 2023, Mhe Hasunga amesema kamati yake imefanya ziara kwenye mradi huo ili kujiridhisha endapo fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya ujenzi wa mabweni hayo zimetumika kama ilivyokusudiwa.
“Baada ya kupata taarifa ya CAG pamoja na taarifa ya mradi kutoka kwa Katibu Mkuu, tumeyaona majengo ya mabweni na yako kwenye hali nzuri yanapendeza na yamekamilika kwa asilimia karibu 100,”amesema.
Aidha,kamati hiyo imeiagiza Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha samani kwa ajili ya mabweni hayo zinapatikana haraka ili mabweni hayo yaanze kutumika kama ilivyokusudiwa.
Kamati hiyo pia imeaigiza Wizara hiyo kuhakikisha samani za chuo hicho na nyingine zinazotumika kwenye vyuo vya VETA nchini zinatengenezwa na VETA kwa kuwa Mamlaka hiyo ina wataalamu wa kutosha kwenye vyuo vyake wenye ujuzi wa kutosha kufanya kazi hiyo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga amesema Wizara yake itafanyia kazi maelekezo ya Kamati hiyo na kuhakikisha fedha kwa ajili ya kutengeneza samani za mabweni hayo takribani shilingi milioni 54 zinapatikana kabla ya kumalizika kwa mwezi Machi, 2023 ili VETA iweze kutengeneza samani hizo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, amesema mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.07 na kuahidi kuwa Wizara yake itahakikisha mabweni hayo yanatunzwa Ili yanufaishe watanzania wengi.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa kamati ya Bunge kwa niaba ya Katibu Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema kukamilika kwa mabweni hayo kutaongeza udahili katika chuo hicho kwa nafasi za bweni kutoka walimu tarajali 120 hadi 216.
Amesema mpango wa VETA ni kuongeza udahili wa walimu tarajali kufikia wanafunzi 660 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025/26 ambapo wanafunzi 320 watapata mafunzo ndani ya chuo (incampus) na 340 ni wanafunzi watakaopata mafunzo kwa njia ya masafa.
0 Comments